Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema kuwa licha ya uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia saba kwa zaidi ya muongo mmoja, bado hali ya uchumi ni mbaya Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ameyasema hayo katika ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa takwimu jijini Dar es Salaam, Dkt. Mpango amesema ili kupambana na umaskini, Serikali imejikita kwenye ujenzi wa viwanda kwa ajili ya kuongeza ajira.
Aidha, ametaja takwimu za Benki ya Dunia (WB) za mwaka 2013 akisema asilimia 10.7 ya watu wote duniani ambao ni bilioni 7.1 walikuwa wakiishi chini ya Dola 1.90 za Marekani kwa siku ikilinganishwa na asilimia 12.4 mwaka 2012.
“Mbali na takwimu hizo kuonyesha umaskini kushuka kwa kasi ndogo, mafanikio hayo hayaonekani waziwazi kwa baadhi ya nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania,” amesema Mpango.
Hata hivyo, amesema kuwa hali hiyo inatokana na ukuaji wa uchumi kutokana na sekta zinazo ajiri watu wachache na nyingi zikijikita mijini na kuwapo kwa kasi ya ongezeko la watu.