Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ngazi ya Maafisa Waandamizi umeanza kufanyika leo tarehe 21 Machi, 2021 katika Hoteli ya Four Points, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Huduma za Jamii katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Christophe Bazivamo amebainisha umuhimu wa Mkutano huo kuangazia maeneo ya msingi ambayo yakifanyiwa kazi na nchi wanachama, yataifanya Jumuiya kufikia lengo la kuwa na maendeleo endelevu katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula kwa viwango vilivyokubaliwa katika Mpango Kamili wa Maendeleo ya Kilimo Afrika.
Ameyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni kuweka na kutekeleza mikakati ya kuboresha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, kuwawezesha na kuwahimiza wanawake na vijana kuchangamkia fursa zinazopatikana kwenye sekta ya kilimo na kuhimiza matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye kilimo ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao.
“Nimatumaini yangu haya machache niliyo yabainisha hapa, na mengi ya muhimu ambayo wataalamu mtajadili kwa kina katika mkutano huu yatachangia kwa kiasi kikubwa kuchochea kasi ya ukuaji wa kilimo na kuleta mabadiliko chanya katika ustawi wa pamoja na kuboresha maisha ya Wanaafrika Mashariki,” alisema Bazivamo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mkutano huo Dkt. Mary Mwale kutoka Jamhuri ya Kenya akirejea takwimu zilizotolewa na Ripoti ya tatu ya Mpango Kamili wa Maendeleo ya Kilimo Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Programme – CAADP) ya mwaka 2022 amewahimiza wataalamu wa kilimo katika Jumuiya kuzisaidia Serikali kuongeza nguvu na ubunifu katika kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo ambayo imeajiri asilimia 80 ya Idadi ya watu wote katika Jumuiya.
Ripoti ya miaka mitatu ya CAADP iliyotolewa mwezi Machi 2022 imebainisha kuwa ukanda wa Afrika Mashariki isipokuwa Jamhuri ya Rwanda hajafikia malengo yaliyoafikiwa kwenye mpango wa Afrika wa kufikia mabadiliko ya kilimo, uzalishaji mali, usalama wa chakula na lishe, ukuaji wa uchumi, na ustawi kwa wote.
“Jumuiya tuna kazi kubwa ya kufanya kwenye Sekta ya Kilimo, tunawajibu mkubwa wa kuhakikisha maendeleo ya kilimo yanakuwa endelevu na yenye tija, ni muhimu pia kukumbuka kuwa 70% ya viwanda vya Jumuiya ya Afrika Mashariki vinategemea sekta ya kilimo, vikiwemo vya uzalishaji wa pembejeo za kilimo; wakati huo huo 65% ya bidhaa zinazouzwa katika Jumuiya zinatokana na kilimo na bidhaa za kilimo,” alisema Dkt. Mwale.
Mkutano huu wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utafanyika katika ngazi tatu, ngazi ya Wataalamu Waandamizi tarehe 21 na 23 Machi, Ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 24 Machi, na mwisho ngazi ya Mawaziri tarehe 25 Machi 2022.
Mkutano huu wa siku tano utakaofanyika kwa njia ya mseto yaani video na ana kwa ana kuanzia tarehe 21 hadi 25 Machi 2022, unatarajiwa kuangazia masuala mbalimbali katika sekta ya kilimo yanayolenga kuhakikisha maendeleo endelevu katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula ndani ya Jumuiya, umehudhuriwa na nchi zote sita (6) wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.