Watendaji wa taasisi zinazohusika na uratibu na usimamizi wa kemikali hapa nchini wameagizwa kusimamia na kudhibiti kemikali hatarishi ikiwa ni pamoja na kuratibu usafirishaji, usambazaji na matumizi ya kemikali hizo.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina Mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na Watendaji hao, amesema kuwa taasisi zinatakiwa kutoa taarifa za utendaji wa kila kazi kila robo ya mwaka kwa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira Nchini (NEMC)
“Nawaagiza kuwasilisha takwimu za kemikali zinazozalishwa nchini, zinazoagizwa au kusafirishwa nje ya nchi, pamoja na kuainisha viwanda vinavyozalisha kemikali vilivyo sajiliwa na maghala yaliyosajiliwa kuhifadhi kemikali hizo” amesema Mpina.
Aidha, Mpina ameagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini, Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania, Tume ya Nguvu za Atomiki, Taasisi ya Utafiti ya Viuatilifu katika Kanda za Kitropiki, Mamlaka ya Chakula na Dawa, OSHA na Mkemia Mkuu wa Serikali kwa pamoja kuandaa Hati ya Makubaliano ya kuratibu utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuhuisha Sheria zao na kupeleka mapendekezo Serikalini ya vifungu vya kufanyiwa marekebisho.
Hata hivyo, Taasisi alizokutana nazo ni pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Nchini (NEMC), Taasisi ya Nguvu za Atomiki, Mamlaka ya Chakula na Dawa na Mkemia Mkuu wa Serikali.