Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina ameipongeza Miradi ya taasisi za Muungano Kisiwani Pemba, kwa kile alichodai, kutekelezeka kwa asilimia kubwa na kutatua kero za wananchi.
Mpina amesema hayo Kisiwani Pemba katika ziara yake ya kutembelea na kukagua baadhi ya miradi inayotekelezwa chini ya taasisi za muungano na mashirika ya TASAF na MIVARF, ikiwa ni pamoja na miradi ya ujenzi wa Soko, Barabara, Hospitali, Shule, Ujenzi wa Mabwawa, Matuta kama makingio ya maji ya chumvi yanayosaidia kuhimili madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha, Mpina amewataka wakazi wa Kaskazini na Kusini Pemba kwa Pamoja kushirikiana na kuitunza miradi hiyo inayotekelezwa kwa thamani ya shilingi za kitanzania Bilioni 14.297, na kusema kuwa ina manufaa kwa wakazi hao.
Katika Ziara yake kisiwani Pemba, Mpina ametembelea jengo la Makazi ya Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Kusema kuwa jengo hilo linatakiwa kutengewa fedha maalumu kwa ajili ya ukarabati.