Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kimesema kitaanza kukamata magari yote ambayo yamewekwa taa zenye mwanga mkali (spotlights) kwa kuwa uwekaji wa taa hizo, ni kinyume na sheria ya usalama barabarani.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Naibu Kamisha Mohammed Mpinga, ambapo amesema ukamataji wa magari hayo utaanza rasmi wiki ijayo.
Mpinga amesema wameshatoa maelekezo kwa askari wa usalama barabarani, kuhakikisha wanakamata magari, pikipiki na malori makubwa ambayo yamewekwa taa hizo.
“Ziko taa za aina fulani zinazowekwa kwenye magari na hata ukitembea usiku utaona mwingine ameweka taa moja mwingine anaweka nyingi sana, kiasi ambacho zimesababisha matatizo kwa madereva wengine,” amesema Kamanda Mpinga.
Aidha, amesema kwenye barabara kuu kuna mtindo wa madereva wa magari makubwa, kuweka taa kubwa ambazo zinawekwa juu na kumulika mwanga mkali, kiasi ambacho dereva anayemulikwa anapata upofu wa muda na kushindwa kudhibiti chombo chake ambapo anaweza kusababisha ajali.