Mpinzani wa Yanga katika mchujo wa kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika anatarajiwa kujulikana leo mchana katika droo itakayopangwa mjini Cairo, Misri yalipo makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Droo hiyo itahusisha timu zilizovuka hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho dhidi ya zilizotolewa kwenye hatua kama hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu zilizotolewa Ligi ya Mabingwa zitamenyana na zilizosonga mbele Kombe la Shirikisho katika michezo ya nyumbani na ugenini kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Michezo ya kwanza inatarajiwa kucheza wikiendi ya Aprili 7 hadi 9 na marudiano yanatarajiwa kuwa wikiendi ya Aprili 14 hadi 16, mwaka huu.
Timu zilizovuka hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho ni MC Alger, JS Kabylie za Algeria, Recreativo do Libolo ya Angola, ASEC Mimosas ya Ivory Coast, El Masry, Smouha ya Misri, MAS Fes, Ittihad Tangier za Morocco, Rayon Sports ya Rwanda, Hilal El Obeid ya Sudan, Mbabane Swallows ya Swaziland, Platinum Stars, Supersport United za Afrika Kusini, Club Africain, CS Sfaxien za Tunisia na Zesco United ya Zambia.
Zilizotolewa Ligi ya Mabingwa ni RC Kadiogo ya Burkina Faso, AC Leopards ya Kongo, AS Tanda ya Ivory Coast, TP Mazembe ya DRC, Gambia Ports Authority ya Gambia, Horoya ya Guinea, CNaPS ya Madagascar, AS Port Louis ya Mauritius, FUS Rabat, Wydad Athletic Club ya Morocco, Ferroviario Beira ya Msumbiji, Rivers United, Rangers ya Nigeria, Bidvest ya Afrika Kusini, Yanga SC ya Tanzania ya KCCA ya Uganda.
Yanga SC imengukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa kupata matokeo ya sare ya 0-0 na wenyeji, Zanaco Jumamosi jioni Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, mjini Lusaka nchini Zambia.
Matokeo hayo yanamaanisha Yanga imetolewa kwa bao la ugenini, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.