Hakimu John Mpitanjia anayeendesha kesi ya Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Nchini, Abdul Nondo amegoma kuachia nafasi yake ya kumtetea Nondo akidai kuwa maelezo yaliyotolewa juu ya kuachishwa kwake hayana ushahidi wa kutosha.
Akitoa uamuzi huo mdogo wa Mahakama, John Mpitanjia amesema mahakama ni chombo cha mwisho cha kutenda haki hivyo itaangalia usawa kwa pande zote mbili ikiwa ni sambamba na kutoa haki kwa wakati bila kufungamana na upande wowote.
Siku ya Mei 15, 2018 Nondo aliandikia barua Mahakama ya Wilaya ya Iringa, kumkataa hakimu huyo anayesikiliza shauri lake kwamba anamtilia shaka na ameona aiandike barua ya kumkataa Hakimu huyo kuendelea kusimamia na kutetea kesi yake ili Mahakama itende haki.
Nondo ambaye anashtakiwa kwa makosa mawili ya kudanganya kutekwa na kutoa maelezo ya uongo kituo cha Polisi Mafinga, alisema kuwa haridhishwi na mwenendo wa kesi yake na anazo hoja 5 ambazo ameziwasilisha mahakamani hapo kuomba kubadilishwa kwa hakimu.
Nondo ametaja baadhi ya hoja hizo kuwa ni madai ya Hakimu huyo kukutana na mmoja wa mashahidi na kuwahoji kama wanaendelea kuwasiliana na Nondo, ya pili Nondo amedai katika kila kesi yake inapopelekwa Mahakamani RCO wa Iringa amekuwa akionekana kukutana na Hakimu Mpitanjia kabla na baada ya kesi hiyo, ma tatu amedai kuwa ni mahusiano na mawasiliano mazuri aliyonayo Hakimu wake na upande wa Jamhuri huku akiwa hana mahusiano mazuri na upande wa mshitakiwa.
Aidha mahakama imesema bado inaendelea kusikiliza ushahidi ili kutoa uamuzi wa tuhuma hizo.