Haukuwa msimu mzuri kwa Mshambuliaji wa FC Lupopo, Mtanzania George Mpole kucheza Ligi Kuu ya DR Congo kama ilivyokuwa matarajio yake ya awali, kutokana na ligi hiyo kusimamishwa ghafla.
Mpole ambaye alijiunga na FC Lupopo kupitia usajili wa dirisha dogo akitokea Geita Gold FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, amejikuta malengo yake yanakwama, baada ya kuambiwa na vingozi wao na ligi hiyo imefutwa na sasa wasubiri taarifa upya.
Mshambuliaji huyo amefunguka kinachoendelea kwa sasa wanasubiri maelekezo ya viongozi wao, kisha ajiandae kurejea Tanzania hadi wakati mwingine na wataambiwa warudi kambini kwa ajili ya msimu mpya (2023/24).
Mpole aliikuta timu hiyo inashiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika hata hivyo hakuicheza michuano hiyo kwani alikuwa ameishaichezea Geita Gold katika michezo ya hatua za awali msimu huu 2022/23.
“Matarajio yangu ya kucheza kwa mafanikio yameingia dosari, kwanza nimekuta timu inacheza michuano ya CAF, ambayo nisingeruhusiwa kucheza, hivyo muda mwingi nilikuwa jukwaani, ingawa nilikuwa nafanya mazoezi na timu.”
“Wakati huo ligi ilikuwa imesimama kupisha michuano ya CAF, hatujakaa sawa Ligi Kuu inafutwa, nimegundua kwa nini wachezaji wengi wa Congo wanapenda kucheza nje na nchi yao, kwani huku nimeziona changamoto nyingi.”
“Ndio maana siwezi kuzungumzia ushindani ama kutofautisha Ligi Kuu Bara na huku kwani bado sijaiona labda kwa wakati mwingine nitakapopata nafasi ya kucheza.”
Ligi ya DR Congo ilikuwa inachezwa na timu 20 na kinara ni AS Vita na katika mechi 10 imeshinda tisa, sare moja na ina alama 28, FC Lupopo anayoichezea Mpole, ipo nafasi ya pili, imecheza michezo tisa, imeshinda saba, sare moja, imefungwa moja ina alama 22.
Timu ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo ni Maniema imecheza mechi nane, imeshinda sita, sare moja na imepoteza mmoja, ina alama 19 na TP Mazembe yenye alama 15 imecheza mechi tisa, imeshinda nne, sare tatu na imefungwa miwili na ipo nafasi ya nne. Kuna uwezekano mkubwa Lupopo wakashiriki tena michuano ya kimataifa mwakani kutokana na nafasi yao waliyomalizia.