Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema uwepo wa Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere visiwani Zanzibar ni kielelezo Chanya katika kuenzi na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa Vitendo.
Hayo yemesemwa na Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Rais Dkt. Hussein Mwinyi katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kampasi ya Karume Zanzibar.
Ameleza kuwa, Bodi pamoja na uongozi wa chuo hicho wamekuwa wakifanya kazi nzuri kwani tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mnamo mwaka 1961 mpaka sasa chuo kimekuwa kinaishi kwa mawazo ya waasisi wa Taifa la Tanzania Hayati Mwalimu J.K Nyerere na Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume.
Amesema, niukweli usiopingika wahitimu wanaotoka katika chuo hicho baada ya kumaliza mafunzo yao hutoka wakiwa wameiva , wenye uwadilifu na uweledi wa hali ya juu jambo ambalo lina umuhimu kwa watu ambao hupewa dhamana katika nafasi za utumishi wa Umma.
Makamu wa Pili wa Rais amemtaka mkandarasi wa mradi huo ambaye ni SUMA JKT kukamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa kwani mradi huo unalenga kutatua changamoto kubwa iliopo kwa wanafunzi ya kukosa makaazi.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Simai Mohamed Said ameupongeza uongozi wa Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuhakikisha yale malengo waliojiwekea ya kutoa mafunzo ya uongozi na uzalendo kwa jamii yanafikiwa.
Aidha, Simai aliukumbusha uongozi wa Chuo hicho mbali na mafunzo ya uongozi na uzalendo wanayoyatoa lakini pia ipo haya yua kuangalia upya uwezekano wa kuwafanya wanafunzi wawe na uwezo wa kufanya vitu vingi kwa pamoja kwa kuzingatia masuala ya Ubunifu na Uvumbuzi kama zinavyofanya nchi nyengine Duniani.
Naye Mkuu wa chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila ametumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa jitihada anazoendelea katika kukuza uchumi wa Zanzibar.
Hata hivyo amegusia changamoto zinazokikabili chuo hicho kwa kampasi ya Karume Zanzibar amesema kumekuwepo kwa changamoto ya baadhi ya watu kuvamia eneo la chuo tangu mwaka 2018 na kumuomba mgeni rasmi kulipatia ufumbuzi suala hilo kutokana na kurejesha nyuma jitihada za chuo hicho.