Serikali nchini, imesema kutekelezwa kwa mradi wa Reli ya kisasa (SGR), kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Kindu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia Gitega nchini Burundi, kutaongeza ufanisi katika matumizi ya Ukanda huru wa biashara Barani Afrika, kwa kuimarisha usafirishaji wa abiria na mizigo.
Hayo, yamebainishwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango wakati akiongoza majadiliano na wawekezaji kuhusu mradi wa reli hiyo ya kisasa, majadiliano yaliofanyika katika Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika linalofanyika Jijini Abidjan nchini Ivory Coast.
Amesema, Serikali zote tatu zimeweka nia ya dhati ya kutekeleza mradi huo ambapo kwa upande wa Tanzania tayari imekwisha tekeleza miradi unganishi ya reli ya kisasa inayochagiza uwepo wa mradi huo muhimu.
Aidha, Dkt. Mpango amesema asilimia 50 ya mizigo inayotoka katika bandari za Tanzania hupelekwa nchi za Burundi na Kongo, hivyo uhitaji wa reli hiyo ya kisasa ni muhimu kwa sasa na kwamba uwepo wa idadi watu inayokadiriwa kufikia milioni 170 katika mataifa ya Tanzania, Kongo na Burundi ni uhakika wa soko kwa bidhaa mbalimbali zitakazosafirishwa kupitia reli hiyo.