Eva Godwin – Dodoma.
Serikali Nchini, imewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya sekta ya Ardhi katika kipindi cha maandalizi ya bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa yale maeneo yasiyotengewa fedha za mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi.
Hayo yanesemwa hii leo Novemba 28, 2023 na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa wakati wa Mkutano wa Kitaifa wa Wadau Kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika Jijini Dodoma.
Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote Nchini zinazotekeleza mradi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa timu zinazotekela mradi katika maeneo yao na kusema “ili mradi ufanikiwe ni vyema wadau wakashiriki kikamilifu katika mradi na nihimize kuhusu wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri kutoa ushirikiano kwa timu za utekelezaji mradi.”
Hata hivyo, amehimiza Taasisi zinazofanya kazi na mradi kama vile NIDA, NEMC, Tume ya Matumizi ya Mipango Bora ya Ardhi na taasisi zote kutoa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi.
“Wataalamu wa sekta ya ardhi kuhakikisha pia wanashirikiana na na viongozi wa serikali za mitaa na vijiji katika kuwapa wananchi elimu kuhusu masuala ya ardhi hususani zile taarifa za utekelezaji mradi,” alibainisha katika hotuba hiyo Silaa.
Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga alisema, mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi mbali na mambo mengine utajenga ofisi zitakazozingatia mahitaji ya mifumo ya kielektroniki sambamba na kujenga madarasa ya kujifunzia kwenye vyuo vya Ardhi vya Morogoro na Tabora.