Mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Shilingu 69 Bilioni, unaojengwa eneo la Butimba jijini Mwanza umefikia asilimia 94 na utaanza majaribio ya kutoa maji Septemba 15 mwaka huu.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo kutaongeza upatikanaji wa maji kutoka lita milioni 90 kwa siku za sasa hadi kufikia lita milioni 138.
Amesema mradi huo utanufaisha wakazi wa maeneo ya Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Nyamazobe, Nyahingi, Buganda, Luchelele, Lwanhima, Sahwa, Fumagila, Kishiri na Igoma kwa upande wa Jiji la Mwanza.
Kwa upande wa Wilaya ya Misungwi alitaja maeneo ya Usagara, Nyashishi na Fella wakati kwa upande wa Magu ni Kisesa, Bujora na Isangijo.