Mradi wa Utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi Tanzania (TACIP) umetambulishwa rasmi Mkoani Morogoro, utambulisho ambao umefanywa na timu ya TACIP akiwemo Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA), Adrian Nyangamalle na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza kwenye kikao kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Kebwe Steven Kebwe.
Katika kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuhudhuriwa na uongozi wa juu wa Mkoa huo akiwemo Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Kazimoto, Ujumbe wa TACIP ulielezea madhumuni mahusi ya Mradi na adhma ya kuwafikia Wasanii wote nchini katika tasnia hiyo kwa lengo la kuwabaini na kuwatambua ili kuwaunganisha na fursa mbalimbali zitakazo tatua changamoto zinatowakabili.
Uongozi wa Mkoa ulifurahishwa na jitihada zinazofanywa na Shirikisho la Sanaa za Ufundi nchini linaloshiriana na Kampuni ya DataVision International katika kutekeleza Mradi huo unaosimamiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia BASATA ambapo Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Kayanza Peter Pinda ndiyo mlezi wa TACIP.
Uongozi wa Mkoa wa Morogoro umeonyesha shauku kubwa na kuunga mkono jitihada hizo na kuahidi kutoa ushirikiano utakaohitajika ili malengo ya TACIP hususani katika Mkoa wa Morogoro yakapate kutimizwa kwa kiwango kikubwa.
Timu ya TACIP akiwemo Rais wa TAFCA, Adrian Nyangamalle, Mkurugenzi wa (Idara ya) Ukuzaji Sanaa BASATA, Vivian Nsao Shalua, Afisa Sanaa mwandamizi na Mkuu wa Matukio BASATA, Ng’oko Malegesi na Afisa Sanaa BASATA, Aurelia Doto waliwatembea wasanii wa kata ya Dumila Wilayani Kilosa na kufanya nao kikao kilichohudhuriwa pia na Mwenyekiti na Mtendaji wa kata hiyo.
Baada ya Mkutano huo ambapo ulihudhuliwa na wasanii zaidi ya 100 timu ya TACIP ilipata fursa ya kutembelea maeneo ya Wasanii ili kujifunza na kubaini changamoto zinazowakabili.
Wasanii wa Dumila walifurahia sana ujio wa TACIP iliyotambulishwa kwao na Gozbetha Rwezaula na kuonyesha matumaini juu ya mabadiliko makubwa yanayoenda kufanyika kwenye sekta ya Sanaa nchini kupitia mradi huo utakao wapa heshima ya kutambulika katika Taifa lao na nje ya mipaka ya nchi.
Baadhi ya changamoto ambazo wasanii wa Dumila waliomba zikapewe kilaumbele na Mradi ni pamoja na, Kero za maafisa misitu zinazopelekea kufanya kazi zinazotokana na malighafi ya misitu kuwa ngumu na kwa kujigicha, Upatikanaji na usafitishaji wa mazao ya miti kama vinyago na fenicha, Mahitaji ya bima ya Afya, Usumbufu na urasimu wa kujisajili BASATA, Masoko hafifu, Mikopo ya mitaji na vifaa na Umoja na sehemu maalum ya kufanyia kazi.
Timu ya TACIP ilichukuwa changamoto hizo na kuahidi kuzifanyia kazi huku ikisisitiza wasanii hao kutimiza wajibu wao kwa kujiandikisha na kuhakikisha kila mmoja anakuwa na kitambulisho chake huku timu hiyo ikisistitiza umuhimu wa Serikali ya kata kutenga eneo maalum kwa ajili ya uzalishaji na soko la Sanaa hasa maamuzi ya serikali kuhamia Dodoma yatumike kama fursa adhimu kwa Wasanii wa Dumila.
Uongozi wa kata uliahidi kutenga eneo maalum kwaajili ya kuweka kituo cha Sanaa Dumila na kuanza mara moja uhamasishaji wa uundwaji wa vikundi vya Wasanii wanotambulika ili wapatiwe fursa mbalimbali ikiwemo ya sehemu ya kufanyia kazi.
TACIP ni mradi wa utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi Tanzania ambao umeanzishwa na kampuni ya kizawa ya DataVision International iliyoko jijini Dar es Salaam, inayojishughulisha na masuala ya Teknlolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Tafiti na Mafunzo, ambapo wanatekeleza mradi huo kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA) chini ya Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo. Mlezi wa mradi huo ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.