Mabingwa wa Soka Tanzania Bara, Young Africans tayari wameanza kambi na mazoezi ya kuanza kwa msimu mpya ‘pre Season’ maeneo ya Kigamboni huku Kocha Mkuu, Miguel Angel Gamondi, akija na mbinu mpya ya kuwapa stamina na kuchezea mpira kwa wakati mmoja.

Mratibu wa Klabu hiyo, Hafidh Salehe, amesema kuwa kocha Gamondi kama wengine na yeye amekuja na mpango mkakati wake wa kuwataka wachezaji kwanza kuuchezea mpira uwanjani, halafu baadaye anaanza mazoezi ya kuwajaza pumzi na stamína, hasa ikizingatiwa kipindi hiki ambacho wachezaji wametoka mapumzikoni.

“Pre season’ kila mwalimu ana mbinu zake, zamani miaka hiyo wachezaji mkirejea kutoka kwenye mpumziko ni mbio tu kama wiki nzima hakuna kugusa mpira, walimu wanajenga stamina na pumzi kwa sababu wachezaji walikuwa mapumzikoni miili imejaa, makocha zamani walikuwa wanaona hiyo ni mbinu pia ya kuwapunguza uzito kwani baadhi yao wanakuwa wamenenepa, baada ya wiki moja ndiyo watu wanagusa mpira, mazoezini na katika mechi za kirafiki,” amesema mratibu huyo.

Hata hivyo, alisema kwa sasa soka limebadilika duniani kote na kila kocha anakuja na mbinu zake mpya za ufundishaji inapoanza pre season.”

“Sasa hivi soka limebadilika sana kama unavyoona mwalimu wetu mpya amekuja na staili ya kuacha wachezaji wanacheza soka kidogo, halafu wanajaza pumzi, kama nilivyotangulia kusema kila tunapozidi kusonga mbele, soka duniani linabadilika,” amesema mratibu huyo wa siku nyingi kwenye klabu hiyo.

Kuhusu mikakati yake, Hafidh amesema kocha wao aliwasisitizia watu wote walio kwenye benchi lake la ufundi nidhamu na ushirikiano.

“Kocha alituita akatuambia mikakati yake, anachozingatia ni nidhamu na ushirikiano, anasema tumechukua makombe mara mbili na fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kwa hiyo timu 15 zilizo nyuma yetu zitakuwa zimepania kutuondoa kwenye utawala kwa hiyo lazima tushirikiane, wachezaji wawe na nidhamu na yeye tumpe ushirikiano, tunaweza kusonga mbele,” amesema.

Young Africans imeanza mazoezi yake ikiwa na kocha mpya, pamoja na baadhi ya wachezaji watano mpaka sasa iliyowasajili kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano.

Wachezaji hao ni Kouassi Attohoula Yao, beki wa kulia, raia wa Ivory Coast, akitokea Klabu ya ASEC Mimosas ya nchini humo, Maxi Mpia Nzengeli kutoka Maniema FC ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Beki wa kati raia wa Uganda, Gift Fred kutoka SC Villa ya Uganda, Nickson Kibabage akitokea Singida Fountain Gate, na Jonas Mkude ambaye aliachwa na Klabu ya Simba SC.

Mashujaa FC kuvuka Bahari ya Hindi
Kocha Simba SC afichua kinachoendelea Uturuki