Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, Augustine Mrema amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutowafumbia macho bodaboda wanaovunja taratibu zilizowekwa kwa kufanya biashara katika eneo la Posta, katikati ya jiji hilo.

Akizungumza jana na madereva bodaboda wilaya ya Kinondoni jijini humo, Mrema alisema kuwa ingawa kuna katazo la Serikali kwa bodaboda kuwa katika eneo hilo bado kunaonekana vituo vya bodaboda ambavyo vinafumbiwa macho, huku baadhi ya wanaojaribu kuingia mjini wakitiwa nguvuni.

“Pikipiki ziko pale katikati ya mji, umenyamaza. Wewe Makonda, usije kusema kijana wangu … nimekwambia. HakyaMungu, nitakusemea mpaka uwaondoe wale watu,” alisema Mrema.

Augustine Mrema akizungumza kwenye mkutano wake na Bodaboda wilaya ya Kinondoni

Augustine Mrema akizungumza kwenye mkutano wake na Bodaboda wilaya ya Kinondoni

Katika hatua nyingine, Mrema aliwataka bodaboda kutokubali kutumiwa na wanasiasa kushiriki katika maandamano na vitendo vingine vinavyovunja sheria ya nchi ili waepuke kutiwa mbaroni na kufungwa jela.

Nao madereva hao walimueleza Mrema kuwa wamekuwa wakinyanyaswa na watu wanaojiita polisi jamii ambao wamekuwa wakiwakamata bila kufuata utaratibu na wakati mwingine kusababisha ajali. Walisema kuwa watu hao ambao hawana mafunzo ya kipolisi, wakati mwingine huwabambikizia makosa ambayo sio yao bali ni ya abiria.

“Unakuta dereva ana helmet amevaa, halafu amempa nyingine abiria ambaye yeye ameamua kuishikilia, lakini dereva ndiye anaeonekana kuwa ana kosa,”alisema mmoja wa madereva hao.

Naye mwenyekiti wa Bodaboda wilaya ya Kinondoni, Almano Mdede alitoa wito kwa bodaboda wote kuwa walinzi wa wenzao katika kuhakikisha hawavunji sheria.

“Na nataka hata wenyeviti wengine wa Tanzania nzima walidake hili. Kwa mambo ambayo yako ndani ya uwezo wetu tunayaona kama kutovaa helmet, tuchukue hatua kali,” alisema Mdede.

Bilionea Sabodo aitosa Chadema, atangaza kuwekeza trilioni 11 Dodoma
Uturuki yakamata Makomando waliotaka kumteka Rais