Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amekiri kupokea barua toka kwa msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi inayowataka kutoa maelezo juu ya maandamano yaliyofanyika Februari 16, 2018.

Na amesema kuwa kila kilichoandikwa katika barua hiyo kitapata majibu kwa kuzingatia sheria taratibu, kanuni na maadili ya vyama vya siasa.

Ameongezea kuwa maandamano ni haki ya vyama na kwa mujibu wa sheria ya Vyama vya siasa na kanuni zake pamoja na katiba ya nchi wamepitia vifungu vyote na hawajaona kosa na kama kutakuwa na kosa la jinai amesema suala hilo halitakuwa chini ya msajili bali litakuwa ni suala la polisi.

”Maandamano ni haki ya vyama kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, kanuni zake na katiba ya nchi, kama ameiona jinai yoyote, hilo ni suala la polisi siyo yeye tena” amesema Mrema.

Hivyo Mrema amesema watajibu barua hiyo ya msajili ambaye pia ni mlezi wa vyama vyote kabla ya muda uliowekwa ili wawe ndani ya muda.

Februari 16, 2018 Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho walifanya maandamano kuelekea kwa Msimamizi wa Uchaguzi kudai barua za utambulisho wa mawakala wao waliosimamia uchaguzi uliofanyika Februari 17.

Kufuatia maandamano hayo, Tanzania inasikitika kumpoteza kijana mdogo ambaye alikuwa mwananfunzi wa chuo cha Usafirishaji aliyepigwa risasi ya kichwa akiwa kwenye basi akielekea Bagamoyo na kufariki dunia, mazishi ya mwanachuo huyo, Akwilina Akwiline yanafanyika leo nyumbani kwao Kilimanjaro kijijini kwake Rombo.

 

Tamko la Zitto baada ya kutoka selo
Alichoamua Mutungi maandamano ya Chadema yaliyomsababishia kifo Akwilina