Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Augustine Mrema ameonesha kushangazwa na maswali aliyotupiwa na waandishi wa habari saa chache baada ya Rais John Magufuli kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole.

Mrema ambaye miezi michache iliyopita alionekana kumkumbusha hadharani Rais Magufuli kuhusu ahadi yake kabla ya kutimizwa jana, amewataka waandishi wa habari kutomuonea kwa kumuuliza maswali ambayo wameshindwa kuwauliza watu wengine kama Rais Magufuli na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Akijibu swali alilouliezwa na mwandishi wa habari kama ataachana na uenyekiti wa chama chake ili aitumikie nafasi hiyo ya uteuzi, Mrema alisema kuwa anaweza kufanya kazi zote kama wanavyofanya Rais Magufuli na Mbowe.

“Si unagawa kazi… wewe vipi bwana! Mbona Rais Magufuli atakuwa Mwenyekiti wa CCM, ni Mkuu wa Nchi, Mkuu wa Majeshi… mbona huyo hamumuulizi kwamba ana kazi nyingi mnakuja kunionea mimi. Mimi sitaki ‘unaa’ bana, mimi zote ntafanya na ntabeba. Ng’ombe azidiwi na nundu yake,” alisema Mrema.

Akizungumzia kupewa nafasi hiyo kama mpinzani, alisema kuwa wanachama wake wanapaswa kujiona wenye bahati kwani sasa Mwenyekiti wao ana chanzo cha mapato ambayo yatamsaidia pia kufanya shughuli za chama kirahisi kwani chama hicho hakipati ruzuku kutokana na kukosa mwakilishi Bungeni.

“Sasa nimepata uwezo, hata wa nikimpa karani anichapie barua pale TLP.. Si pesa ninazo. Kwanza mimi nilikuwa sina kitu, nimepewa uwezo sasa vipi wanachama wa TLP waanze kunung’unika,” anakaririwa.

Alisema baada ya mwezi mmoja tu hali ya utendaji wake katika chama utaimarika kwani hivi sasa amepewa uwezo. Hivyo, aliwataka wanachama wa chama hicho waliokuwa wamekihama kurudi kundini.

Picha: Walichofanyiwa Wanajeshi waliofanya jaribio la Mapinduzi Uturuki
Bavicha watangaza kukutana tena Dodoma kivingine