Serikali ya Marekani imemfungulia mashtaka mrembo wa Urusi mwenye umri wa miaka 29 kwa tuhuma za kufanya upelelezi na kuingilia mifumo ya siasa kwa lengo la kuivuruga nchi hiyo.
Mrembo huyo aliyetajwa kwa jina la Maria Butina amedaiwa kutengeneza uhusiano mzuri na kufanya kazi kwa karibu na chama cha Republican na kwamba amekuwa mwanaharakati wa kutetea haki za kumiliki silaha, kwa mujibu wa BBC.
Maria anatuhumiwa kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na ofisi ya Mueller, akiwasiliana na baadhi ya maafisa waandamizi wa Marekani.
Hata hivyo, Mwanasheria anayemtetea Butina, Robert Driscoll amekanusha tuhuma hizo na kudai kuwa mteja wake sio wakala wa kijasusi wa Urusi bali ni mwanafunzi wa wa Chuo Kikuu anayechukua masomo ya Mahusiano ya Kimataifa ambaye anataka kutumia Shahada yake katika masuala ya biashara za kimataifa.
Aliongeza kuwa mteja wake hajawahi kujaribu kuwashawishi watu wa aina yoyote kuzifuata au kuzipinga sheria na sera za Marekani na kwamba amekuwa akishirikiana kwa ukaribu na maafisa wa Serikali kuhusu tuhuma zinazomkabili.
Butina ambaye anaishi Washington, Marekani alikamatwa Jumapili iliyopita na ameendelea kushikiliwa mahabusu akisubiri kupandishwa kizimbani Jumatano wiki hii, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Haki (DOJ).
Taarifa za kukamatwa kwa msichana huyo zimewekwa wazi muda mfupi baada ya Rais Donald Trump kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin. Katika mkutano huo Trump aliitetea Urusi kuhusu tuhuma za kuingilia uchaguzi wa mwaka 2016.
FBI wameeleza kuwa baada ya kumfuatilia, walibaini kuwa alikuwa anafanya kazi ya kushawishi kukubalika kwa Urusi pia miongoni mwa maafisa waandamizi wa Marekani na kuanzisha taasisi za kiharakati kinyume na kibali chake cha kuingia nchini humo.
Alianza kundi la kutetea haki za kumiliki silaha aliloliita ‘Bear Arms’ na pia alikuwa na uhusiano wa karibu na National Riffle Association.
Aidha, ripoti ya FBI imesema kuwa walibaini Butina alikuwa anaripoti maendeleo ya kazi yake kwa Serikali ya Urusi kupitia jumbe za moja kw amoja za Twitter (Twitter direct messages).
Mrembo huyo ambaye asili yake ni Serbia, anadaiwa kuwa alihudhuria pia mikutano ya Trump na kupata nafasi ya kumuuliza maswali, akitaka kujua msimamo wake kuhusu uhusiano wa Marekani na Urusi.