Msanii wa muziki wa asili, Mrisho Mpoto kwa kushirikiana na timu yake ya ‘Mpoto Foundation’ ametembelea na kutoa zawadi katika kituo cha watoto yatima cha Mwandaliwa na madrasa ya Tidaiya iliyopo Tandale.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akikabidhi zawadi hizo, Mpoto amesema lengo kubwa la kutoa zawadi hizo ni kusaidia malezi ya watoto katika vituo hivyo ili wakue wakiwa katika maadili mazuri.
“Nimeamua kugawana na watoto kidogo nilichojaliwa nacho ili waweze kufurahi lakini pia kuwasaidia katika makuzi hasa kwenye suala zima la kidini na maadili.” amesema Mpoto.
Mpoto ameongeza kuwa kutokana na mambo mengi yanayoendelea kwa sasa nchini na duniani kote, kuna uwezekano kwa watoto kukua bila misingi mizuri ya dini, heshima na uzalendo kama wasipoandaliwa mazingira mazuri.
Ili kuhakikisha hilo halitokei, Mpoto amesema imekuwa sababu kubwa iliyompelekea kujitolea zawadi hizo ambapo kwa yeye ni kuufungua mwaka 2018 akiwa na thawabu kutoka kwa watoto.