Magwiji wa Klabu za Simba SC na Young Africans, Edibily Lunyamila na Dua Said wameanika mtego ulioachwa na Fiston Mayele wakidai unaweza kumtesa Mshambuliaji anayesajiliwa kuziba pengo la Mkongomani huyo anayeondoka.
Young Africans inatarajia kuanza maisha bila huduma ya Mayele aliyemaliza akiwa kinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara sambamba na Saido Ntibazokiza wa Simba SC kila mmoja akifunga mabao 17 na pia kinara wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kutokana na kuuzwa Pyramids ya Misri.
Wakati mashabiki wakitamani kufahamu mrithi ataletwa kutoka nje kuchukua nafasi ya Mayele, mastaa wa zamani akiwamo pia Abdallah Kibadeni wamefunguka namna Young Africans ilivyoachiwa mtihani na Mshambuliaji huyo aliyefunga jumla ya mabao 33 katika Ligi Kuu kwa misimu miwili.
Kiungo Mshambuliaji ‘Winga’ wa zamani wa Young Africans na Simba SC aliyetamba pia Malindi na Taifa Stars, Lunyamila amesema kumpata mbadala wa Mayele ni ngumu kwani hakuwa na mpinzani kikosini, hivyo ni lazima anayekuja awe mkali zaidi yake.
“Young Africans haitabomoka kumkosa mtu kama Mayele kwani ina viungo wengine na kuondoka kwake ni jambo sahihi na itawapa nafasi waliopo kuonyesha kile walichoku- wa nacho,” amesema.
Dua amesema mrithi wa Mayele anatakiwa kufanya makubwa zaidi ya Mshambuliaji huyo, kwani atakuwa akiangaliwa sana ili kuona nini anafanya.