Mrithi wa kiti cha Ubunge cha jimbo la Singida Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Miraji Mtaturu ameapishwa Bungeni leo katika kikao cha kwanza cha mkutano wa 16 Bunge la 11, ulioanza leo Jijini Dodoma.

Kabla ya kuapishwa, alisindikizwa mbele na wabunge wengine kwa shangwe, na baada ya kuapishwa Spika wa Bunge, Job Ndugai akatoa neno la pongezi na kuwahakikishia kuwa wananchi wa Singida Mashariki wamepata muwakilishi halali, “sasa wananchi wa singida mashariki wanaye muwakilishi halali Bungeni” amesema Spika Ndugai.

Ameanza kazi rasmi na kuuliza swali la nyongeza kwa wizara ya Maji juu ya mpango wa kutoa fedha za kuhakikisha visima vya maji katika wilaya ya Ikungi vinaanza kutoa maji ili kukabiliana na tatizo la maji wilayani humo.

Mtaturu alishinda kiti cha ubunge wa jimbo la Singida Mashariki bila pingamizi baada ya wagombea wa upinzani kuto rejesha fomu na kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Tundu Lissu baada ya kupoteza sifa za kuwa Mbunge kutokana na kutojaza fomu za mali na madeni na kutoshiriki vikao vya Bunge bila ruhusa.

Ikumbukwe kuwa hadi sasa Lissu amefungua kesi Mahakamani akipinga kuvuliwa ubunge kulikotangazwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye alitangaza kuwa Lissu amekosa sifa za kuendelea kuwa Mbunge kwa kuwa hakuonekana Bungeni na hakutoa taarifa ya maandishi pamoja na kutojaza fomu ya tamko la mali na madeni, na uamuzi wa kesi hiyo unatarajiwa kutolewa septemba 9 mwaka huu.

Lissu anatarajiwa kurejea nchini Septemba 7, mwaka huu kutoka nchini Ubeligiji ambako anapatiwa matibabu ya majeraha yaliyotokana na kupigwa risasi zaidi ya 30, septemba 7, mwaka 2017, nyumbani kwakwe Area D, Jijini Dodoma na watu wasiojulikana.

 

 

 

 

 

Oliver Kahn arejea Bayern Munichen
LIVE BUNGENI: Fuatilia yanayojiri Bungeni Dodoma muda huu leo Septemba 3, 2019