Chama cha ACT-Wazalendo kimemteua Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho bara, Dorothy Semu kukai kaimu nafasi ya Uenyekiti iliyoachwa na Maalim Seif Sharif Hamad ambaye amefariki dunia Februari 17, 2021 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa  Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma, Salim Bimani imeeleza kuwa Semu anachukua nafasi hiyo kwa mujibu wa  ibara ya 84(3) na (4) ya katiba ya ACT- Wazalendo ya mwaka 2015 toleo la mwaka 2020.

Ibara ya 84(3) ya Katiba ya ACT- Wazalendo ya mwaka 2015 toleo la mwaka 2020 inasomeka: iwapo Mwenyekiti wa chama hayupo kwa sababu yoyote ile basi Makamu Mwenyekiti anayetoka upande mwengine wa Muungano tofauti na anaotoka Mwenyekiti, na kama Makamu Mwenyekiti aliyetajwa kwanza naye hayupo, basi Makamu Mwenyekiti aliyebakia atakaimu nafasi ya Uenyekiti”.

“Kwa kuzingatia ibara ya 84(4) ya katiba ya ACT- Wazalendo, Semu ataendelea kukaimu nafasi hiyo ndani ya kipindi kisichozidi 12 hadi pale mwenyekiti mpya atakapochaguliwa na mkutano mkuu maalumu wa taifa wa chama hicho,” imeeleza taarifa hiyo.

Kabla ya kushika wadhifa wa Umakamu Mwenyekiti, Semu aliwahi kuwa katibu mkuu wa ACT-Wazalendo nafasi aliyoiacha mwaka jana katika Mkutano Mkuu ambapo Ado Shaibu alimrithi.

Bobi Wine aondoa kesi ya kupinga matokeo mahakamani
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 23, 2021