Mshambuliaji mpya wa Young Africans, Hafiz Konkoni, ametamba kuisaidia Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans kufanya vizuri, ili kutetea mataji na kutikisa vilivyo kwenye Michuano ya Kimataifa msimu ujao 2023/24.
Konkoni aliyetia saini mkataba wa miaka miwili kuichezea Young Africans, amejiunga na klabu hiyo na kuziba pengo la Fístone Mayele, aliyetimkia Pyramid ya Misri baada ya msimu uliopita kumaliza akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Msimu uliopita, mrithi huyo wa Mayele alifunga mabao 15 katika ligi ya Ghana baada ya kucheza mechi 26 na kutoa pasi tatu za mabao huku akishika nafasi ya pili kwa ufungaji.
Kabla ya Konkoni kusajiliwa Young Africans, alihusishwa kujiunga na klabu ya Al Hilal ya Sudan.
Akizungumza baada ya utambulisho, Konkoni amesema amefurahi kuwa sehemu ya familia ya Young Africans, atapambana na kuisaidia timu kupata matokeo mazuri.
“Nimekuja kufanya kazi na kufanikisha malengo ya klabu, sítabweteka na kulewa sifa bali nitapambana na kushirikiana na wenzangu,” amesema Konkoni.
Mshambuliaji huyo amesema anaushukuru uongozi kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kuitumia Young Africans ambayo hataiangusha kwa kufanya kazi kwa bidii na nidhamu.
Konkoni anakuwa mchezaji mpya wa nane kusajiliwa Young Africans baada ya mabeki Nickson Kibabage (Singida Fountain Gate), Gift Freddy (SC Villa-Uganda), Kouassi Attohoula Yao, viungo, Peodoh Pacôme Zouzoua (ASEC Mimosas ya Ivory Coast).
Wengine waliomwaga wino Jangwani ni kiungo Jonás Mkude (Simba), Mahlatse Skudu Makudubela (Marumo Gallants-Afrika Kusini) na Maxi Mpia Nzengeli (AS Maniema Union-DRC).