Kiungo Mkabaji mpya wa Simba SC, Abdallah Hamis ameshukuru mapokezi makubwa aliyoyapata ndani ya timu hiyo, huku akiahdi kubeba mataji yote watakayoshindania katika msimu ujao.
Kauli hiyo huenda ikawa kijembe kwa Watani wao wa Jadi, Young Africans ambao ndio Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Ngao ya Jamii waliopanga kuyabakisha mataji yote hayo katika msimu ujao.
Nyota huyo alitambulishwa juzi Alhamisi (Julai 20) mara baada ya kukamilisha taratibu zote za usajili ndani ya kikosi cha Mbrazili, Oliviera Robert ‘Robertinho ambacho kimeweka kambi nchini Uturuki.
Hamis amesajiliwa kwa ajili ya kuja kuchukua nafasi ya aliyekuwa kiungo wa Simba SC, Jonas Mkude ambaye ametambulishwa Young Africans hivi karibuni, akisaini mkataba wa mwaka mmoja.
Hamis amesema kuwa, ana kibarua kigumu cha kuhakikisha anaipa mafanikio timu yake hiyo mpya aliyojiunga nayo kwa mkataba wa mwaka mmoja.
“Asanteni wote mashabiki wa Simba SC kwa mapokezi yenu. Nimekuja katika klabu hii kubwa kushinda makombe na hatutakubali kuchukua nafasi ya pili katika msimamo wa ligi msimu ujao.
“Lengo letu kuu ni kufanikiwa ndani na nje ya uwanja na kuonyesha nidhamu bora na uongozi bora. Kwa kushirikiana na mashabiki wa Simba SC, ninaamini tunaweka historia msimu ujao,” amesema Hamis.