Historia kuandikwa leo. Ndivyo unavyoweza kusema wakati wajumbe zaidi ya 700 wa Mkutano Mkuu wa dharura wa CUF watakapomchagua mwenyekiti mpya wa chama hicho kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu wadhifa huo Agosti mwaka jana.
Profesa Lipumba aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani kuanzia 1995 hadi mwaka jana, aliachia ngazi kwa kile alichodai kupinga uamuzi wa viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Baada ya profesa huyo wa uchumi aliyegombea urais mara nne kujiweka kando, CUF iliunda kamati ya watu watatu chini ya uenyekiti wa Twaha Taslima, kukiongoza chama hicho hadi hapo utakapofanyika uchaguzi mwingine wa viongozi.
Katika uchaguzi huo utakaofanyika katika ukumbi wa Blue Pearl, atapatikana mwenyekiti mpya na kuingia katika kumbukumbu ya kuwa mwenyekiti wa nne wa chama hicho.
Waliowahi kuwa wenyeviti wa chama hicho ni Profesa Lipumba, Musobi Mageni na James Mapalala.
Wanao gombea  uenyekiti ni Abdul Omary Zowo , James Mahangi , Joseph Rhobi , Juma Nkumbi , Salum Barwany, Selemani Khatibu, Zuberi Kuchauka, Riziki Mngwali na Twaha Taslima.
Wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti ni Dk Juma Ameir Muchi, Juma Duni Haji, Mussa Haji Kombo na Salim Abdallah Bimani.
Chama hicho kilionekana kama kitayumba baada ya Profesa Lipumba kujiuzulu, lakini kilivuka kigingi hicho na katika Uchaguzi Mkuu uliopita kilishinda viti 10 vya ubunge Tanzania Bara, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kilipoanzishwa.
Hata hivyo, chama hicho, kwa upande wa Zanzibar hakikupata nafasi ya wabunge wala uwakilishi baada ya kususia uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20.
Uchaguzi huo wa marudio ulifanyika baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015

Watu 30 Wauawa Na Wengine 90 Wajeruhiwa Nchini Uturuki
Ole Sendeka Awatahadharisha Chadema Kuhusu Mchezo Wanaotaka Kuwachezea Watanzania