Miraji Mtaturu (CCM), Mbunge mpya wa Singida Mashariki aliyekalia kiti hicho baada ya Tundu Lissu (Chadema) kutangazwa kuwa amekosa sifa za kuendelea kuwa mbunge wa jimbo hilo, anatarajia kuapishwa kesho, Septemba 3, 2019 bungeni jijini Dodoma.

Ratiba ya Mkutano wa 16 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaoanza kesho, iliyotolewa na Ofisi ya Bunge inaonesha kuwa pamoja na mambo mengine, Mtaturu atakula kiapo cha uaminifu mbele ya Spika.

Mtaturu alitangazwa kuwa mshindi wa ubunge wa jimbo hilo baada ya watu waliokuwa wamechukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kutoziwasilisha ndani ya muda uliokuwa umepangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Juni 28, 2019 Spika wa Bunge, Job Ndugai alitangaza kuwa jimbo la Singida Mashariki liko wazi na kwamba ameshamuandikia barua Mwenyekiti wa NEC na kumuelekeza kuitisha uchaguzi.

Spika Ndugai alisema amefikia uamuzi huo kwakuwa Lissu amevunja kanuni na sheria za Bunge kwa kutojaza fomu ya mali na madeni ya viongozi wa umma pamoja na kutohudhuria mikutano zaidi ya mitatu ya Bunge bila kutoa taarifa kwake (Spika).

Lissu ambaye alikuwa nchini Ubelgiji akipatiwa matibabu kufuatia tukio la kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana, Septemba 7, 2017 jijini Dodoma, amefungua kesi ya kupinga uamuzi wa Spika Ndugai. Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu.

Mbwana Samatta ‘awashika’ waliomtoa Cristiano Ronaldo

Dullah Mbabe, Vifua viwili watamba ughaibuni
Mbwana Samatta ‘awashika’ waliomtoa Cristiano Ronaldo