Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini Sisty Nyahoza, ameviasa vyama vya siasa vinavyotaka kuungana Oktoba 3 mwaka huu, kuacha mara moja mpango huo kwani wanakiuka utaratibu wa sheria na kwamba ni vyema kila mmoja akaendelea kunadi sera zake.

Nyahoza ametoa kauli hiyo leo Oktoba Mosi, 2020, wakati akizungumza na kituo kimojawapo cha redio jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa tayari ofisi ya msajili wa vyama vya siasa imeshaviandikia barua vyama hivyo kwa kuwa ni masuala ya kiofisi huwa hawaziweki barua hizo hadharani.

“Kwanza tunaawaasa hao wanaotaka kufanya hivyo tarehe 3 sisi kama walezi wa vyama vya siasa kwa sababu wanakiuka sheria, walianza vizuri hivyo kila mmoja aendelee kunadi sera yake na wagombea wao wa urais”, amesema Nyahoza.

Amesema sheria ya vyama vya siasa inawekwa kwa maslahi ya wanachama na wananchi na unapotaka kushirikiana hutakiwi kufanya kitendo chochote kinachohadaa wananchi kwa hiyo ni kosa kufanya hivyo ghafla wakati wa uchaguzi.

“Ukiunganisha nguvu na chama kingine wakati mmeshakubaliana na wananchi kwamba mtatekeleza sera gani ni kuwahadaa, sisi tulishawasiliana nao na tukawaambia waache,” ameongeza Nyahoza.

Vyama vya siasa vya upinzani vya ACT-Wazalendo na Chama Cha Demokrasia na Mandeleo (CHADEMA), vimekuwa vikitajwa kuwa na mpango wa kumuunga mkono mgombea mmoja wa urais Oktoba 3, licha ya kuwa vyama vyote hivyo vimeshasimamisha wagombea wao wa urais.

TAKUKURU yaokoa zaidi ya shilingi Bilioni 1
Shibuda :Sera ya majimbo ni chanzo cha mifarakano