Msajili wa vyama vya siasa nchini ametakiwa kufuatilia mwenendo wa vyama vya siasa nchini na kukifutia usajili chama chochote cha siasa kinachokiuka sheria na taratibu zilizopo.
Kauli hiyo imetolewa jana Bungeni na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kupitia mwenyekiti wake, Mohamed Mchengerwa, alipokuwa akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusu hotuba ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri Mkuu na ofisi za Bunge kwa Mwaka wa Fedha 2018/19.
Aidha, Mchengerwa aliitaka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kufanya ukaguzi wa matumizi ya ruzuku kwa vyama vya siasa ili kuhakikisha fedha hizo hazifanyiwi ubadhilifu.
“Kamati inashauri Ofisi ya Vyama vya Siasa kuzingatia sheria, kanuni, utaratibu na weledi katika usimamizi na utoaji wa ruzuku kwa vyama vya siasa,” alisema Mchengerwa.
Akizungumzia maoni ya kamati yanayomtaka msajili kuvifuta vyama vya siasa visivyozingatia kanuni na sheria, Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson alisema kuwa nakala ya hotuba hiyo itawasilishwa kwa Msajili kwani ushauri uliotolewa na kamati hiyo ni mzito.
- Walioathiriwa na sakata la Facebook wafika milioni 87
- Aliyekuwa Rais wa Brazil kutumikia miaka 12 jela kwa ufisadi
Katika hatua nyingine, kamati hiyo iliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha inafanya kazi zake kwa weledi na kuwachukulia hatua watumishi wake wanaofanya uzembe wakati wa usimamizi wa chaguzi ili kuepuka migogoro isiyo na tija.
Kamati hiyo iliitaka Tume kuwashirikisha wadau wote wakati wa uhuishaji wa taarifa za wapiga kura katika daftari la wapiga kura.