Msajili wa Vyama vya Siasa nchini amekipa siku saba Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoa maelezo kwanini kisichukuliwe hatua kwa kutofanya uchaguzi wa viongozi wake wa kitaifa licha ya kipindi cha uongozi wao kikatiba kuisha.
Barua ya Msajili iliyosainiwa Oktoba Mosi mwaka huu, imewaeleza Chadema kuwa wamekiuka sheria kwa kutoitisha mkutano mkuu wa chama na kufanya uchaguzi wa viongozi wapya kwani muhula wa miaka mitano wa viongozi wa kitaifa waliopo uliisha tangu Septemba 14, 2019.
Msajili ameeleza kuwa anatilia shaka sababu za kutoitisha mkutano mkuu zilizotolewa na Chadema kupitia barua zao za awali kwenda kwenye Ofisi yake, akieleza kuwa hakuna taarifa ya wao kulalamika kwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa Polisi wamezuia kufanyika kwa mikutano yao ya ndani.
“Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa hatujawahi kusikia na wala hatuna taarifa kwamba CHADEMA mliwahi kuwasilisha malalamiko kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuhusu madai yenu ya kukataliwa na Jeshi la Polisi kufanya vikao vyenu vya ndani vya Uchaguzi, ”imeeleza barua ya Msajili.
“Kifungu cha 43 (6) cha Sheria ya Jeshi la Polisi sura ya 322 kinaeleza kuwa malalamiko ya kukataliwa na Jeshi la Polisi kufanya mkutano au kikao yawasilishwe kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani,” imeongeza barua hiyo.
Barua hiyo imekariri Katiba ya Chadema vinavyoeleza kuwa uchaguzi wa viongozi wa kitaifa utafanyika kila baada ya miaka mitano na kwamba huo ndio utakuwa ukomo wa kipindi cha uongozi ndani ya chama hicho.
Aidha, imekariri Katiba ya Chama hicho ambayo inaeleza kuwa kiongozi ambaye atashindwa kuitisha vikao vya kikatiba vya chama atakuwa hajatimiza majukumu yake.
“Hivyo, Chadema mnapaswa kuwasilisha maelezo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, kwanini msichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa, Katiba na Kanuni zenu. Maelezo yenu yawasilishwe Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa siyo zaidi ya tarehe 07 Oktoba, 2019 saa tisa na nusu mchana,” imeeleza barua hiyo ya iliyosainiwa na Sisty L. Nyahoza kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa.