Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Mohamed Nabi, ameutaka Uongozi wa Klabu hiyo kuwa makini na kuchukua tahadhari zote kuelekea mchezo wa Kufuzu Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
Young Africans itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam Jumatano (Novemba 02), kisha itakwenda Tunisia kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili katika jiji la Tunis.
Taarifa kutoka Young Africans zinaeleza kuwa, Kocha huyo amesisitiza utayari kuelekea mchezo huo, ili kufanikisha malengo ya kufuzu na kutinga Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho.
Hata hivyo mmoja wa viongozi wa Young Africans amekiri kuwepo kwa mpango wa kutimizwa kwa maagizo ya Kocha Nabi, huku akiweka wazi namna walivyoanza kuyafanyia kazi.
Kiongozi huyo amesema kila mmoja klabuni hapo amedhamiria hawarudii makosa walioyafanya wakati walipocheza dhidi ya Mabingwa wa Sudan Al Hilal kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
“Tayari maagizo yote ya Kocha Nabi yameanza kufanyiwa kazi, Uongozi umemtaka Kocha kujiandaa upande wa timu na kuhakikisha anatuvusha kutupeleka hatua ya makundi,”
“Tumejipanga kwa kila kitu, tumeshatuma jopo la watu kwenda Tunisia ili kuweka mambo sawa kabla ya timu yetu haijaenda huko kwa mchezo wa Mkondo wa Pili, safari hii tutahakikisha tunafanikiwa na kuendelea kuwa sehemu ya timu zitakazoshiriki Kimataifa kutoka Afrika Mashariki na Kati.” amesema kiongozi huyo
Young Africans iliangukia Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kufungwa 2-1 na Mabingwa wa Sudan Al Hilal, iliyotinga hatua ya Makundi na kujiunga na timu nyingine 15 katika hatua hiyo.
Timu zilizofuzu kuchza hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ni Al Ahly(Misri), Espérance de Tunis (Tunisia), Wydad Casablanca, Raja Casablanca (Morocco) Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Zamalek (Misri), Petro de Luanda (Angola), AC Horoya (Guinea), Simba SC (Tanzania), CR Belouizdad (Algeria), JS Kabylie (Algeria), AS Vita Club (DR Congo), Coton Sport (Cameroon), Al Merrikh (Sudan) na Vipers (Uganda).