Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania imetangaza kusitisha msako wa Rubani Samweli Balina Gibuyi aliyepotea na ndege ya PAMS Foundation inayotumiwa na hifadhi za taifa.
Mamlaka hiyo imetangaza hivyo baada ya kutopata taarifa yoyote kwenye msako huo uliofanyika kwa wiki kadhaa kwa kutumia anga na ardhini kuyatazama maeneo yote ambayo yalikua yanatajwa kuwa huenda angekutwa huko.
Ndege hiyo ndogo iliyosajiliwa nchini Tanzania kama 5H-MXO aina ya Bat Hawk iliripotiwa kupotea tarehe 18 October 2021 baada ya kuondoka katika kiwanja kidogo cha Matemanga Wilayani Tunduru saa tisa alasiri kuelekea kiwanja kidogo cha Kingupira kilichopo Hifadhi ya Selous kwa lengo la kufuatilia mienendo na usalama wa wanyamapori hasa Faru weusi.
Ndege hiyo ilipoondoka ilikuwa na Rubani pekee na haikuwasiliana na kituo chochote cha kuongozea ndege wala haikuweza kuonekana kwenye mitambo ya kuangazia ndege kwasababu ilikuwa ikiruka chini sana
Taarifa ya Mamlaka ya anga Tanzania imesema utafutaji wake utaendelea pale itakapopata taarifa zinazoashiria upatikanaji wa ndege au Rubani wake.