Raia wawili wa kigeni wamekamatwa jana jijini Dar es Salaam kwa kosa la kufanya kazi kinyume cha sheria.
Afisa Ajira na Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Yusuf Nzugile ameviambia vyombo vya habari kuwa msako uliofanywa na ofisi hiyo ulibaini kuwa raia hao wa kigeni walikuwa wanafanya kazi katika kampuni ya Shelys Pharmaceuticals.
Alieleza kuwa mmoja kati ya watuhumiwa hao alibainika kuwa na kibali cha kufanya kazi ambayo ni tofauti na kazi aliyokuwa anafanya kwenye kampuni hiyo, huku mwenzake akiwa hana kibali cha aina yoyote.
“Tunapotoa kibali cha kazi kwa mfanyakazi ambaye ni raia wa kigeni, tunategemea awe anafanya kazi ambayo inaonekana kwenye kibali chake, vinginevyo atakuwa anavunja sheria,” alisema Nzugile.
Akielezea kuwa kibali cha mtuhumiwa wa kwanza kinaonesha kuwa alikuwa anafanya kazi kama afisa manunuzi lakini mkataba wake unaonesha ameajiriwa kama mkemia.
Akizungumzia hatua hiyo ya Serikali, Meneja Rasilimali Watu wa kampuni hiyo, Nissa Mwaipyana alikiri kukamatwa kwa wafanyakazi hao na kueleza kuwa hali ya utofauti wa kazi na vibali ilitokana na kucheleweshwa kwa vibali licha ya kuwasilisha maombi.
Hata hivyo, alikiri kuwa kampuni hiyo imevunja sheria na kwamba waliamua kufanya hivyo kutokana na uhaba wa wafanyakazi katika idara ya kemikali.