Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewaasa wasanii wa muziki wa kizazi kipya kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utunzi wa tungo za nyimbo zao ili kuepuka mikwaruzano baina yao wenyewe na wakati mwingine na Serikali.
Mwakyembe ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa pole kwa msanii Ibrahim Mussa maarufu kama ‘Roma Mkatoliki’ na wenzake watatu waliokuwa wametekwa na watu wasiojulikana na kusema kuwa Serikali ina nia njema ya kulinda watu na mali zao.
“Ni wajibu wa kila msanii wa muziki kuzingatia kanuni,taratibu na sheria wakati wa utunzi wa nyimbo ili kuepusha migongano na watu mbalimbali na Serikali na hivyo kuendeleza ushirikiano na mshikamano kwa matokeo chanya kwa jamii” amesema Dkt.Mwakyembe.
Aidha Waziri Mwakyembe amewahakikishia wasanii kuimarisha masuala mbalimbali yanayohusu tasnia ya sanaa ili waweze kufanikiwa kibiashara na kukuza soko la tasnia hiyo ndani na nje ya nchi.
Pia Mwakyembe amewataka wananchi kuacha kutoa taarifa za upotoshaji kuhusu ukweli wa suala hilo la utekwaji nyara wa wasanii hao na badala yake kusubiri taarifa sahihi kutoka katika vyanzo husika.
Kwa upande wake msanii wa kizazi kipya, Ibrahim Mussa maarufu kwa jina la Roma Mkatoliki ameipongeza na kuishukuru Serikali na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwa karibu na wasanii ikiwemo jitihada walizoonyesha kuhakikisha kuwa yeye pamoja na wenzake wanapatikana wakiwa salama.
“Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali , viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, wasanii wenzangu na wananchi kwa ujumla kwa ushirikiano wao wa dhati wa ” amesema Msanii Roma.
Hata hivyo, Msanii Ibrahimu Mussa na wenzake watatu walitoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu tarehe 5 Aprili mwaka huu na baadaye kupatikana siku ya Jumamosi tarehe 8 Aprili mwaka huu wakiwa na majeraha ambayo yaawasababishia maumivu makali.