Napoleon, mmoja kati ya wanafamilia wa kundi la Outlawz la marehemu Tupac, amewashtua mashabiki wa rapa huyo kwa kudai kuwa aliyempiga risasi na kumuua jijini Las Vegas sio anayetajwa kuhusika.
Inaaminika kuwa Tupac aliuawa na kundi la kihalifu la West Coast mwaka 1996; na kwamba aliyefyatua risasi ni moja kati ya wanafamilia wa kundi hilo, Orlando Anderson aka Baby Lane.
Hata hivyo, Napoleon ambaye jina lake halisi ni Mutah Wassin Shabazz Beale, ameibuka na kudai kuwa Baby Lane sio mtu aliyefyatua risasi.
Baadhi ya wasanii wa kundi la Outlawz walikuwa kwenye gari ambalo Tupac alipigwa risasi, akiwemo Yaki Kadafi ambaye anadaiwa kumtambua mhusika.
Katika video ambayo ameweka YouTube, Napoleon anadai kuwa Kadafi aliyekuwa kwenye gari moja na Tupac, alimtazama vizuri mtu aliyefyatua risasi zilizomuua Tupac. Kwa kuwa Kadafi anamfahamu Baby Lane, Napoleon amedai kuwa aliyemuona sio Baby Lane.
- Basata kupokea na kukagua nyimbo kwa WhatsApp
- 50 Cent amrukia Ashanti baada ya kuuza tiketi 24 tu za tamasha lake
“Kadafi alimuona muuaji wa Pac. Alituambia kuwa yule muuaji alimuangalia kwanza kama mtu mwema, lakini baadaye alimuona anatoa mkono kupitia dirishani akiwa na bunduki,” alisema.
“Walishuhudia, Outlawz walikuwepo lakini Kadafi ndiye aliyemuona vizuri yule jamaa. Huyo jamaa alimuangalia Kadafi, na Kadafi alimuangalia kabla ya kuanza kufyatua risasi,” aliongeza.
Aliongeza kuwa Kadafi hakutegemea kama mtu huyo angefyatua risasi hadi alipomuona akitoa mkono kupitia dirishani.
“Inabidi muelewe tunapotoka kwa nyakati zile, ambapo Kadafi alisema hataki kufanya kazi na polisi kuhusu tukio lile. Kwanini hakuwaambia polisi? Ile ilikuwa lugha ya ishara ya mitaani,” alisema Napoleon.
“Wakati ule, tulipotoka hakukuwa na kamera za aina hii kama sasa, au Instagram useme ngoja nikaangalie kwenye akaunti yake nione kama ni yuleyule niliyemuona,” Napoleon aliongeza.
Tupac alipoteza maisha Septemba 13, 1996 alipokuwa hospitali akipatiwa matibabu ya majeraha yaliyotokana na shambulizi la Septemba 7.
Hadi leo, polisi hawakuwahi kumtoa hadharani mtuhumiwa wa mauaji ya Tupac au muuaji wa hasimu wake wa kimuziki, Notorious B.IG aliyeuawa Machi 9, 1997 kwa kupigwa risasi pia.
Wakati huo, Kadafi alisema kuwa anamfahamu vizuri mtu aliyempiga risasi Tupac endapo akimuona na kwamba alikuwa ndani ya gari jeupe lililopaki karibu yao.
Hata hivyo, miezi miwili baada ya tukio hilo, Kadafi aliuawa na binamu yake Napoleon, ambaye alijisalimisha polisi katika tukio ambalo jeshi hilo lilidai kuwa alimpiga risasi kichwani kwa bahati mbaya.
Alitumikia kifungo cha miaka nane na kuachiwa baadaye.