Eva Godwin – Dodoma.

Bohari ya Dawa – MSD, imeanza rasmi kutekeleza jukumu la usambazaji wa bidhaa za afya mara sita badala ya mara nne kwa mwaka, kwa vituo vyote vya umma vya kutolea huduma za afya nchini, huku ikitarajia kutoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 200.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu na Waandishi wa Habari hii leo Agosti 7, 2023 jijini Dodoma Hassan Ibrahim amesema hatua hiyo imetokana na mapitio ya mnyororo wa ugavi na mapendekezo ya maboresho ya usambazaji bidhaa za afya.

Amesema, “usambazaji huu umeondoa changamoto za upatikanaji wa bidhaa za afya ukilinganisha na mfumo wa awali wa kusambaza kila baada ya miezi mitatu, yaani mara nne kwa mwaka na ikumbukwe MSD inasambaza bidhaa za afya hadi mlangoni mwa vituo vya kutolea huduma za afya nchi nzima kuanzia ngazi ya Zahanati hadi hospitali.”

Hata hivyo, amesema katika kufanikisha ongezeko la uzalishaji wa bidhaa za afya nchini na kuendana na azma ya Serikali ya uanzishaji wa viwanda, MSD ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha miundombinu ya kiwanda cha mipira ya mikono kilichopo Idofi Mkoani Njombe na kuanza uzalishaji ndani ya mwaka huu wa fedha 2023/24.

“Kiwanda hiki kinatarajiwa kuzalisha takribani jozi 86,400,000 za mipira ya mikono kwa mwaka na kitachagiza uzalishaji wa malighafi ya mpira kutoka maeneo tofauti Nchini, uzalishaji huu utapunguza utegemezi wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi na kuokoa matumizi ya fedha za kigeni kiasi cha shilingi bilioni 33 kwa mwaka,” amesema Ibrahim.

Dkt. Tax apokea Hati za utambulisho UNICEF, UNDP waaga
Bigirimana apigwa chini Young Africans