Kocha Mkuu wa Klabu ya Young Africans, Mbelgiji, Luc Eymael, ameweka wazi kuwa amepanga kumsajili mshambuliaji raia wa Ubelgiji, Andréa Fileccia, 28, anaekipiga katika Klabu ya Royal Francs Borains ya nchini Ubelgiji katika kipindi cha Dirisha kubwa la usajili kwa ajili ya kuimarisha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Ikumbukwe kuwa, kwa sasa Eymael yuko nchini Ubelgiji ambapo alirejea baada ya Ligi Kuu Bara kusimamishwa kutokana na mlipuko wa maambukizi ya virusi vya Corona.
Eymael aliniambia kuwa, amepanga kumsajili mshambuliaji huyo ambaye atakuja kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Young Africans na tayari aliwaachia viongozi wa klabu hiyo jina la mchezaji kwa ajili ya kukamilisha dili hilo mapema kabla ya kuingia kambini kujiandaa na ligi ya msimu ujao.
Eymael aliongeza kuwa, dili hilo huenda likakamilika kirahisi kwa sababu amewahi kumfundisha mchezaji huyo wakati yupo Afrika Kusini.
“Unajua Yanga inahitaji kuwa na mshambuliaji ambaye ni hatari sana kwa timu pinzani, na nimepanga kumsajili mshambuliaji raia wa Ubelgiji, Andréa Fileccia ambaye kwa sasa anacheza hapa Ubelgiji na tayari nimeshawapa mapendekezo yangu viongozi wa Yanga kuwa namuhitaji mchezaji huyo kwa ajili ya msimu ujao.
“Kukamilisha uhamisho wake naona itakuwa ni rahisi kwa sababu nimewahi kumfundisha wakati niko Afrika Kusini na mimi sioni kama dili hilo linaweza kukwama kwa kuwa nafahamiana vizuri sana na Fileccia na tunaongea vizuri “. Alisema Eymael.