Vita ya kuwania Ubingwa wa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu mpya wa mwaka 2023/2024 inatarajia kuanza rasmi kesho Jumanne (Agosti 15) katika viwanja vitatu tofauti.
Mechi za ufunguzi wa ligi hiyo ni kati ya Ihefu SC dhidi ya Geita Gold FC wakati Namungo FC wakiwa nyumbani kwao kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi wataikaribisha JKT Tanzania iliyorejea tena Ligi Kuu wakati Dodoma Jiji nao watawavaa Wagosi wa Kaya, Coastal Union.
Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi, amesema kikosi chake kiko tayari kuanza msimu mpya na anafahamu utakuwa mgumu, wenye ushindani, lakini anaipa nafasi timu yake kufanya vizuri kutokana na aina ya kikosi walichonacho.
Itakuwa ngumu, naweza kutabiri nani atakuwa bingwa mwanzo tu wa msimu, lakini natarajia ligi ngumu na yenye ushindani, nikizungumza kutokana na kikosi changu, tuna nafasi ya kufanya vizuri na kutetea ubingwa wetu.” amesema Gamondi.
Gamondi amesema pamoja ya kuwa na kikosi kizuri, hii ni mara yake ya kwanza kufundisha katika Ligi ya Tanzania, lakini amejipanga kukabiliana na changamoto zote ili kufikia malengo.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema timu yake imejiandaa kucheza soka safi kwa kuwa ndio utamaduni wa klabu yao pamoja na yeye amekuwa muumini wa ‘SAMBA’.
“Kama timu tumejiwekea malengo yetu, tumefanya usajili mzuri wa kutufikisha kwenye malengo, tumejipanga kuchukua ubingwa lakini tukicheza soka kama ilivyo utamaduni wa klabu yetu, tuko tayari kwa Ligi Kuu,” amesema Robertinho.
Kocha wa Singida Fountain Gate, Hans van der Pluijm, alisema hatarajii michezo rahisi msimu huu kwa sababu timu nyingi zimnefanya maboresho ya vikosi vyao kwa kusajili wachezaji wenye ubora.
“Itakuwa ligi yenye ushindani, kila timu imepata muda mwingi wa maandalizi na zimesajili wachezaji kuimarisha vikosi vyao, kwangu mimi kikubwa ni kuwafanya wachezaji wangu waendelee kucheza katika ubora wa hali.” amesema Pluijm