Moto ulioteketeza soko la Samunge, usiku wa kuamkia jana jumapili, umepelekea kifo cha mfanyabiashara aliyefahamika kwa jina la James Temba (57), mkazi wa Mshono, Jijini Arusha, aliyefariki baada ya kupata mshtuko kutokana na maduka yote mawili kuteketea kwa moto.
Mmoja wa waathirika wa moto huo, Dismas Temba amesema alifika sokoni hapo saa saba na robo usiku na kukuta moto ukiwa umesambaa soko zima huku harakati za kuuzima na kuokoa mali zikiendelea, ndipo James alipofika eneo hilo na kukuta maduka yake mawili ya kuuza vyombo vya ndani na friji yakiwa yameshateketea.
Amesema baada ya James kuona hali hiyo, alipatwa na mshtuko na kuanguka chini kisha kupoteza fahamu hali iliyowalazimu wenzake kumkimbiza Hospitali ya mkoa ya Mount Meru kwaajili ya matibabu.
” Baada ya kufika hapa na kukuta maduka yake mawili yanayouza mafriji na vyombo vya nyumbani yameteketea, alipatwa na mshtuko mkubwa na kuanguka chini kisha kukimbizwa hospitali ambako alifariki dunia” Ameeleza James.
Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Koka Moita, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya mkoa ya Mt. Meru.
Kuhusu chanzo cha moto huo amesema bado hakijafahamika na polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kilichosababisha, huku akibainisha kuwa moto ulianza saa 5 usiku na polisi walifika eneo la tukio kwaajili ya kuzima moto huo.
Hata hivyo amesema amesema kazi ya kuuzima ilikuwa ngumu kwakuwa vibanda vilikuwa vimesongana sana na kujengwa kwa mbao, mabanzi na mabati hivyo kusababisha gari la zimamoto kushindwa kuingia katika vibanda hivyo.