Msichana aliyemuua mumewe kwa kumchoma kisu wakati alipokuwa akijaribu kumbaka, akitaka kukutana naye kimwili kwa mara ya kwanza, amehukumiwa kifo. Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama Kuu ya Sudan.
Noura Hussein mwenye umri wa miaka 19 ambaye alilazimishwa kuolewa na binamu yake akiwa na miaka 16, anadaiwa kumgeuka na kumuua mumewe huyo siku chache baada ya kufungishwa ndoa.
Adhabu hiyo ya kifo imemshukia baada ya ndugu wa marehemu kukataa kupokea fidia ya fedha wakisisitiza kuwa adhabu kali itolewe dhidi ya msichana huyo.
“Familia ya marehemu ilipokea hukumu hiyo kwa furaha na shangwe,” alisema Amal Habani, mwandishi wa habari wa Sudani aliyefika mahakamani kusikiliza hukumu hiyo.
Hata hivyo, watu wanaomuunga mkono msichana huyo walifurika kwenye mahakamani wakiwa na mabango na waliondolewa baadaye kwa nguvu na polisi.
Kwa mujibu wa mmoja kati ya wanaoendesha kampeni ya kumtetea Noura, alilazimishwa kufunga ndoa na marehemu akiwa na umri wa miaka 16.
Imeelezwa kuwa baada ya kulazimishwa kusaini mkataba wa ndoa mwaka 2014, aliondolewa na kwenda kuishi kwenye nyumba ya ndugu yake mashariki mwa Sudan akisubiri sherehe za harusi na kukabidhiwa kwa mumewe.
Wanasheria wa Noura wamepewa siku tatu kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama.
Chanzo: Aljazeera