Wananchi wametakiwa kuacha kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya eneo la mita 60 katika kingo za mito, fukwe za bahari na maziwa ili kuepusha uharibifu wa mazingira huku Serikali inatarajia kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu itakayosaidia katika kutatua changamoto ya mafuriko yanayotokea wakati wa msimu wa mvua katika
maeneo mbalimbali nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis hii leo Novemba 7, 2023 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima aliyetaka kujua mipango wa Serikali kudhibiti Mto Nakasangwe na Tegeta, inayopanuka kwa kasi na kutishia maisha ya watu na mali.
Akijibu swali hilo, Khamis amesisitiza utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 kuhusu Hifadhi ya Eneo la Mita 60 kutoka vyanzo hivyo vya maji inayozuia matumizi yoyote ya kibinadamu katika maeneo hayo na kwamba Serikali itaangalia uwezekano wa kufanya tathmini katika maeneo mengine ambapo ilibuni na kutekeleza miradi ya ujenzi
wa kuta kama vile Pangani na fukwe katika Barabara ya Barack Obama jijini humo.
Amesema, “Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto za kupanuka kwa mito hiyo zikiwemo
kuandaa Mwongozo wa Usafishaji Mchanga, Tope na Taka ngumu kwenye mito na mabonde Dar es Salaam. Ili kukabiliana na changamoto hizi tumeendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa vyanzo vya maji katika ngazi zote.”