Baada ya kimya cha muda mrefu hatimaye Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa ameibuka na kuitaka Serikali kueleza sababu za kuwatumbua watumishi mbalimbali wa Serikali bila hata ya kuwapa nafasi ya kujitetea.
Ameyasema hayo Bungeni Mjini Dodoma mara baada ya kuuliza swali kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) Angella Kairuki kuhusu utumbuaji wa watumishi.
Msigwa amesema kuwa Serikali imekuwa ikitumbua watumishi wa Serikali bila kufuata utaratibu wa kuwapa nafasi ya kujitetea.
Aidha, Msigwa amehoji haki za watumishi wanaotumbuliwa kwa kile alichokiita ni mafungu ya utmbuaji ambao wamekuwa hawapewi haki ya kujitetea.
Hata hivyo, akijibu swali hilo, Waziri Kairuki amesema kuwa kanuni za utumishi wa umma hutekelezwa kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Utaratibu na miongozo na kwa mujibu wa ibara ya 36 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, Rais ndiye mwenye Mamlaka ya mwisho kuhusu usimamizi na uendeshaji wa utumishi wa umma