Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa jana alianza mikutano yake ya hadhara ndani ya jimbo lake baada ya kupewa kibali na Jeshi la Polisi, huku akitamba kuruka viunzi masharti aliyopewa.

Msigwa ambaye pia ni waziri kivuli wa mambo ya nje, aliwaondoa hofu wananchi waliohudhuria mkutano huo, ambao alidai kuwa kwa kuwaangalia anaona wana hofu kutokana na makatazo yaliyotolewa na Jeshi la Polisi.

“Hakuna mtu mwenye mamlaka ya kunipangia cha kuzungumza, sipo hapa kwa matakwa ya polisi. Mimi nipo kwa matakwa ya kisheria na ninazungumza kwa mamlaka mliyonipatia,” alisema Msigwa.

“Pia Katiba inaeleza wazi mad raka na kinga ya Mbunge. Mbunge anayo haki ya kuitisha na kufanya mkutano wa hadhara kwa mjibu wa sheri,” aliongeza.

Moja kati ya masharti aliyopewa Msigwa na Jeshi la Polisi ni kuhakikisha hatoi lugha za kukashfu mtu wa chama kingine au Serikali, na kutomualika mtu yoyote aliye nje ya jimbo lake.

Katika hatua nyingine, Msigwa alikosoa uamuzi uliotangazwa na Rais John Magufuli wa Serikali kuhamia Dodoma, akidai kuwa katika mpango wa Serikali wa miaka mitano na mwaka mmoja uliowasilishwa Bungeni, hakukuwa na kipaumbele cha kuhamia Dodoma.

“Serikali ilileta mpango wake wa miaka mitano, mwaka mmoja na bajeti, hivi vyote vinaletwa bungeni na baada ya kujadiliwa na kupitishwa, vinatungiwa sheria ili viweze kutekelezwa hivyo vipaumbele vyake ni lazima vifiti kwenye mipango hiyo,” alisema Msigwa.

“Lakini katika vyote vitatu vya mwaka huu, mpango wa miaka mitano, mwaka mmoja na hata katika bajeti ya mwaka huu sijaona mahali popote palipoandikwa kipaumbele cha Serikali ni kuhamia Dodoma.

Aliwataka wananchi wa Iringa kuhoji mpango huo wa kuhamia Dodoma utakaoigharimu serikali kiasi kikubwa cha fedha huku akisisitiza kuwa mipango yote huwasilishwa Bungeni na kutungiwa sheria.

Mbali na hayo, Msigwa alizungumzia mpango wa maendeleo jimboni kwake ikiwa ni pamoja na kutengeneza miundombinu na kuboresha huduma za elimu na afya akiwataka wananchi kushirikiana katika kufikia malengo.

Video: NEMC imetangazafaini wananchi wanaokaa karibu na mifereji
Picha: Ziara ya Waziri Mkuu Morogoro, ukaguzi wa miradi ya maendeleo