Na Allawi Kaboyo – Biharamulo.

Mbunge wa jimbo la Biharamulo Magharibi, Mhandisi Ezra John Chiwelesa, amewapa pole waumini wa dini ya Kiislamu wanaotumia Msikiti uliopo mji mdogo wa Nyakanazi, kata ya Rusahunga wilayani Biharamulo, kufuatia mvua iliyoambatana na upepo mkali kusababisha madhara mbalimbali, ikiwemo kuezuliwa kwa paa la Msikiti huo.

Akizungumza wakati alipotembelea Msikiti huo na kujionea hali halisi ilivyo, Chiwelesa amewaomba waumini hao kuwa na subira katika kipindi hiki, huku utaratibu wa kuirejesha nyumba hiyo ya ibada kwenye hali yake ya kawaida ukiwa unaendelea.

Chiwelesa amesema kuwa nyumba za ibaada zinapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa viongozi wa dini wamekuwa wakizitumia mara nyingi, kuwaombea viongozi pamoja na taifa hasa kwenye kipindi cha janga la Corona na hata kipindi cha uchaguzi mkuu.

Aidha, Chiwelesa amesema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo atahakikisha Msikiti huo unarekebishwa na kurudi katika hadhi yake ndani ya wiki moja na kutoa wito kwa wadau mbalimbali  kumuunga mkono ili kuhakikisha nyumba hiyo ya ibaada inasimama upya na waumini wanaendelea na ibada kama kawaida.

Taarifa iliyotolewa na Imaam mstaafu wa Msikiti huo Ustadhi Mbaraka Mrisho, mbele ya Mbunge Chiwalase imeeleza kuwa  mvua hiyo ilinyesha majira ya saa 7 mchana na kusababisha madhara hayo hali inayopelekea sasa ufanyaji wa ibada kusuasua kutokana na hali ya hewa ilivyo kwa sasa.

Mrisho amesema kuwa licha ya kutokea kwa maafa hayo hakukutokea madhara yoyote kwa binadamu hivyo watu wote wapo salama, licha ya kuwa changamoto iliyopo sasa ni namna ya ufanyaji  wa ibada, ambapo ametumia fursa hiyo pia kuwaomba wadau kuweza kuchangia ili msikiti huo urudi katika hali yake ya kawaida.

Kwa mujibu wa Imaam Mrisho, baada ya tathimini kufanyika gharama za kurekebisha Msikiti huo hadi kukamilika kwake, ni zaidi ya shilingi milioni 6.5.

Andre Villas-Boas: Jezi namba 10 istaafishwe
BAVICHA yashauri Mdee na wenzie 18 kutimuliwa CHADEMA