Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa nchini Italia kuja Tanzania kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa kuwa Tanzania ina malighafi za kutosha pamoja na uwepo wa masoko ya uhakika kutokana na eneo la kijiografia.

Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza katika Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia, lilifanyika Palazzo Regione Lombardia, Milan nchini Italia akimuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 – 20, 2023.

Amesema, “msisitizo wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mkakati wa Serikali ni kuwahamasisha wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa mbalimbali nchini waje kuwekeza katika ujenzi na kuzalisha bidhaa hizo nchini ili zipatikane kwa wingi na kwa urahisi.”

Majaliwa ametaja baadhi ya maeneo ambayo wawekezaji hao wanaweza kuja kuwekeza katika sekta za madini, kilimo, mawasiliano, mifugo, uvuvi, utalii na afya hivyo amewakaribisha wafanyabiashara hao na wawekezaji watumie fursa hiyo na kuwekeza nchini.

Amesema, licha ya Tanzania kuwa na maeneo na mazingira mazuri ya uwekezaji pia amesema nchi ina vivutio vingi vya utalii hivyo, amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara, pia Mheshimiwa Majaliwa ameyakaribisha makampuni na mawakala wa utalii waje nchini na kuwekeza katika ujenzi wa hoteli za kitalii katika miji mbalimbali yakiwemo majiji ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma.

Hata hivyo, Majaliwa amesema kwasasa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara, viwanja vya ndege na nishati ya uhakika ili kurahisisha shughuli mbalimbali zikiwemo za uwekezaji.

FAO yavutiwa mradi uwezeshaji Vijana Tanzania
Ufugaji: Tumieni mbinu za kisasa zenye tija - RC Mrindoko