Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimeweka wazi msimamo wake juu ya uamuzi wa Waziri Mkuu wa zamani na aliyekuwa kada mkongwe wa chama hicho kuhamia Chadema hivi karibuni.

Chama hicho kilitoa msimamo wake jana katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye makao makuu yake visiwani humo, mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi wa ngazi ya juu wa chama na serikali wakiwepo Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Kificho na mjumbe wa Kamati Kuu Shamsi Vuai Nahodha.

Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari iliyosomwa na Katibu wa Mkoa wa Mjini, Mohamed Omar Nyawenga, viongozi hao walieleza kuwa wao na wanachama wa chama hicho kwa ujumla hawamuungi mkono Edward Lowassa kwa uamuzi aliouchukua kwa kuwa wanaamini Kamati Kuu ya chama hicho ilitenda haki kuliondoa jina lake kwenye mchakato wa kura za maoni tofauti na anavyolalamika.

Walisema kuwa maelfu ya wanachama wa chama hicho walikuwa wanamuunga mkono kwa sababu alikuwa mwanasiasa mctendaji aliyekifahamu vizuri chama hicho lakini baada ya kuhamia upande wa upinzani hawana sababu tena ya kumuunga mkono.

“Sisi kama wana CCM na maelfu ya wanachama wengine hatukubaliani naye. Wana CCM waliomuunga mkono Lowassa kutoka mikoa mitano ya Zanzibar kwa kuamini kwamba yeye ni kiongozi ambaye amepitia katika uzoefu mkubwa katika chama chake, lakini hawakumuunga mkono kwa sababau ya sura yake wala utajiri wake…hapana,” alisema Katibu wa Mkoa wa Mjini, Mohamed Omar Nyawenga.

Swali ambalo bado ni kitendawili, ni idadi ipi ya wanachama walioamua kutomuunga mkono Lowassa baada ya kuihama CCM? Je, wanachama waliokuwa wanamuunga mkono ni wale ‘CCM- Dam Dam’ na hawamfuati mtu?

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama hicho, Shamsi Vuai Nahodha alisisitiza kuwa CCM ilitenda haki kwa kufuata utaratibu wa kanuni zilizozoeleka kama ilivyofanya mwaka 2005 aliposhinda, Dkt. Jakaya Kikwete.

“Utaratibu huohuo ndio uliotumika mwaka huu wa kuwateuwa wagombea, lakini jambo la kushangaza ni kwamba kuna watu wanasema taratibu zimeekiukwa wakati hakuna kilichobadilika. Utaratibu wetgu sisi ni kumjadili mtu kwa sifa, na kama mtu akiwa na sifa anateuliwa,” alisema Nahodha.

Taarifa hiyo ya CCM- Zanzibar inakuja wakati ambapo watanzania walio wengi wana kiu ya kusikia taarifa ya jumla ya chama hicho hususani kutoka katika uongozi wa ngazi za juu Tanzania Bara.

Hivi karibuni, Lowassa alichukua fomu ya kugombea nafasi ya urais kupitia Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa na kutangaza vita ya kisiasa dhidi ya chama chake hicho cha zamani kuwa watahakikishwa wanakishinda katika uchaguzi mkuu ujao.

Mbunge huyo wa Monduli aliamua kuitosa CCM kwa madai kuwa alionewa na Kamati Kuu ya Chama hicho katika mchakato wa kura za maoni ya kumpata mgombea wa nafasi ya urais, mchakato uliomalizika kwa kumtangaza Dkt. Magufuli kuwa mshindi.

 

Nape ‘Atiririka’ Baada Ya Kushikiliwa Na Takukuru Kwa Tuhuma Za Rushwa
Wasira Azungumzia Tuhuma Za Kumpiga Ngumi Mwenyekiti Wa CCM