Faisary Ahmed – Kagera.

Wazazi wenye watoto wenye ulemavu mkoa wa Kagera wametakiwa kutowaficha watoto wao bali kuwapatia haki yao ya elimu kwa kuwaandikisha shule maalum ifikapo mwaka mpya wa masomo 2024, ili waweze kutimiza ndoto zao na kunufaika na fursa zinazojitokeza ikiwemo misaada inayotolewa kutoka serikalini na kwa wadau wa maendeleo.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Bukoba, Erasto Sima wakati akikabidhi vifaa kwa wanafunzi wenye ulemavu akiwa shule ya msingi Tumaini iliyopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima kwenye picha ya pamoja na wanafunzi wenye uhitaji maalum waliopatiwa baiskeli za miguu mitatu.

Amesema “tusiwafiche watoto nyumbani, tuwapeleke shuleni na tuwatambulishe kwenye maeneo mbalimbali ili waweze kujulikana, unapomficha mtoto unakuwa unamnyima haki zake za kimsingi leo watoto hawa walikuwa wazi wametambulika na wamepata vifaa vitakavyowasaidia.”

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya zoezi la utoaji misaada kwa wanafunzi hao wenye uhitaji maalum, Mtendaji Mkuu wa shirika la TECRA Kagera, Mgisha Kaswadi ameeleza kuwa watoto hao wamepewa misaada hiyo ili iwe somo kwa wazazi wao.

Mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima akikabidhi sare za shule kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum zilizotolewa na shirika la kuwahudumia watu wenye ulemavu TECRA Kagera.

Amesema “leo tumetoa misaada kwa watoto wenye ulemavu tofauti tofauti kutoka kwenye maeneo mbalimbali ndani ya wilaya ya Bukoba na Misenyi ambao tayari wako shuleni”.

Charles Buberwa ni miongoni mwa wazazi wenye watoto wenye ulemavu wa akili amesema kuwa “Serikali naiomba izidi kuweka msisitizo kwa wale wazazi watakao onekana kuwaficha watoto wao ndani wafatiliwe kwasababu sio vizuri kumficha ndani baada ya kumpa haki zake za kimsingi.”

Naye, Almachius Lwekaza ni mwanafunzi mwenye ulemavu anayesomea shule ya msingi Mugeza Mseto ameshukuru kwa msaada huo wa baiskeli ya miguu mitatu na kueleza kuwa itamsaidia kwani mwanzoni amekuwa akipitia changamoto wakati akitaka kwenda sehemu.

Vifaa hivyo vilivyotolewa kwa wanafunzi 50 wenye ulemavu kupitia shirika la TECRA kwa hisani ya watawa wa kike wa Marekani ni sare za shule, viatu, baiskeli, viti mwendo na vifaa vya kusomea vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 17.

Polisi kuendeleza uimarishaji ulinzi kwa watalii
PSG kumng'oa Victor Osimhen SSC Napoli