Shirika la Kimataifa la kutetea haki za Binadamu la Amnesty International, limesema mataifa ya Afrika Magharibi na Kati ni lazima yapambane katika vita dhidi ya ufisadi na kuacha kuwatesa watetezi wa haki za binaadamu wanaofichua uovu na ula rushwa.
Amnesty imeyasema hayo na kutoa mfano wa Mwandishi Habari wa Cameroon, Martinez Zogo, ambaye alikuwa akichunguza tuhuma za ubadhirifu wa mamia ya mabilioni ya fedha za Afrika Magharibi na Afrika ya Kati yanayohusishwa na watu walio karibu na serikali.
Kufuatia uchunguzi huo, Zogo alitekwa nyara na watu wasiojulikana Januari 17, na mwili wake ulipatikana baadae ukiwa umekatwa vikungo vyake katika eneo moja nje ya mji mkuu Yaounde huku Mwandishi mwingine wa Togo, Ferdinand Ayite akikamatwa Desemba 10, 2021, baada ya kuwatuhumu maafisa wawili wa serikali kwa rushwa.
Ayite alihukumiwa Machi 15, Pamoja na mwenzake, kifungo cha miaka mitatu jela na kutozwa faini ya faranga milioni 3 karibu na dola 5,000 kwa kile kilichodaiwa kudharau mamlaka na kueneza propaganda, na walikata rufaa dhidi ya uamuzi huo lakini mwishowe wakalazimika kukimbia nchi wakihofia usalama wao.