Mwenyekiti wa klabu ya Young Africans Mshindo Mbette Msolla ametetea kauli aliyoitoa mwishoni mwa juma lililopita, wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Mwananchi mjini Dodoma Agosti 22, ambapo alisema wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wanatakiwa kuchangia usajili wa wachezaji wawili wa kimataifa ili kukamilisha idadi ya 10.

Kauli hiyo imeibua gumzo mtandaoni, huku wananchi wakitaka kujua kama hao wawili ni miongoni mwa nyota wanaotarajiwa kuja nchini Muangola Fernandes Guimares na Yacouba Sogne.

Kikosi cha Young Africans kilisaliwa na nyota watatu kipa Faruk Shikhalo, Haruna Niyonzima na beki kisiki Lamine Moro huku waliowasili kuungana na wenzao hadi sasa ni Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda na Michael Sarpong.

Msolla amesema kauli yake haikumaanisha kama ilivyopokelewa, bali alikua na maana kuwa ni utaratibu kwa wanachama na mashabiki kuchangia kupitia tamasha la KUBWA KULIKO.

“Tuna nafasi mbili zimebakia ili wafike 10, tuliona kama uongozi tumpe nguvu mdhamini wetu, watu wachangie tukamilishe hao wengine. Hao wawili sio wale ambao tushamalizana nao. Kama hatutafanikisha kwenye usajili huu mkubwa kuna dirisha dogo tutamaliza” amesema Msolla

Kuhusu mkataba wa La Liga na Sevilla, Msolla amesema mwisho wa mwezi huu watapata andiko la kwanza la mfumo tarajiwa wa kuendesha klabu na kitachofuata ni kubadilisha katika ya Young Africans.

“Mwisho wa mwezi huu tutapata andiko la kwanza, tutaitisha mkutano mkuu wa matawi kuwapitisha kwenye andiko la kwanza la katiba pendekezwa na muundo pendekezwa kisha waende kwenye matawi wakajadili kwa wiki tatu” amesema Msolla

Pia akaongeza kuwa rufaa ya sakata la Morrison kwenda Fifa na leo watawasilisha Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kuona wataamuaje.

Katika mkutano huo Msolla amemtambulisha Senzo Mazingisa kuwa mshauri katika timu hiyo kwenye mabadiliko ya muundo wa klabu ambao unahusisha La Liga na Young Africans.

Senzo amesema anafuraha kufanya kazi Jangwani yenye rekodi nyingi na atahakikisha anashiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko na kuleta matokeo chanya.

Lori la mafuta lawaka moto Morogoro.
CUF yatangaza wabunge