Walimu nchini wameaswa kusimamia maadili ya kazi zao kikamilifu ili kulinda taaluma zao na kupata matokeo chanya katika nyanja za kielimu, ufaulu wa wanafunzi na kulipatia Taifa watumishi watakaokuwa Vingozi bora wa baadae.
Sambamba na hatua hiyo pia imebainishwa kuwa malalamiko 512,777 yaliyowasilishwa na watumishi wa Umma kwa Baraza la Mitihani la Taifa ambao vyeti vyao vilifanyiwa ukaguzi ili kutambua uhalali wake katika awamu ya 13, vyeti 15,411 kati ya hivyo vilikutwa ni feki vikiwemo vya walimu.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania Dkt. Charles Msonde ameyasema hayo Jijini Dodoma Oktoba 18, 2019 na katika kikao kazi cha Baraza la Walimu chini ya Chama cha Walimu nchini (CWT), cha kujadili changamoto mbalimbali.
Amesema ufanisi wa zoezi hilo katika kubaini mapungufu ya vyeti hivyo vya watumishi wa Umma umefanikiwa kufuatia uadilifu wa watendaji wa Baraza baada ya kupambana na vishawishi mbalimbali toka kwa walaghai ili kuwakingia kifua kwa manufaa yao binafsi.
“Nawapongeza watumishi wa Baraza waliokuwa na dhamana ya kuhakiki vyeti vya watumishi wa umma kwakweli wamefanya kazi nzuri sana maana wamekumbana na vishawishi vya rushwa ya mamilioni ya pesa na magari huu ni uadilifu mkubwa na una tija kwa Taifa,” amebainisha Msonde.
Aidha amesema udanganyifu katika mambo mbalimbali ya kitaaluma ikiwemo mitihani ya wanafunzi hudhalilisha utu hivyo Walimu wanatakiwa kusimama imara katika kutetea maslahi ya Taifa kiuchumi, kimaadili na hata kiuongozi ili kuleta maendeleo ya nchi kupitia taaluma kwa ngazi ya Msingi, Sekondari na Vyuo.
“Tunapoteza pesa nyingi kutokana na kuvuja kwa mitihani na unapovuja mtihani mmoja ukifutwa ni umepoteza bilioni za pesa na ndio maana Mwalimu akijihusisha na wizi wa mitihani au udanganyifu ni sawa na kujidhalilisha yeye mwenyewe na taaluma yake na hili jambo halifai,” Ameongeza Msonde.
Amesema endapo walimu watasimamia taaluma zao kiukamilifu kwa kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu wa mitihani kwa kuwakabili watu wenye nia ya kuwarubuni ili kuwawezesha watoto wao kufaulu isivyo halali itasaidia kuwepo na manufaa kitaifa kwa kupata walimu viongozi bora wa baadae.
“Mlio na dhamana na mna taaluma wote lazima muhusike katika kusimamia na kusahihisha mitihani na si kutafuta watu walio nje na idara husika ya ualimu licha ya uwepo wa vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo huhakikisha mambo yanaenda kwa uhakika hii ni endapo tunahitaji kusonga mbele,” amefafanua Katibu Msonde.
Msonde ambaye alikuwa ni mgeni Rasmi katika kikao hicho pia amesema ili kutoa motisha kwa Mwalimu na kuongeza ubora wa ufanisi wa kazi zao wanatarajia kutoa tuzo kwa walimu, waratibu elimu, shule na watendaji wa mikoa kwa ushirikiano wa Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI).
Aidha katika hatua nyingine amesema endapo CWT itasimama imara ni wazi kuwa watainua taaluma nchini kwani vitendo vya udanganyifu huleta madhara kwa Taifa na kudai kuwa Serikali haitapuuza jambo lolote ambalo litawasilishwa kwa Baraza kama taarifa kutoka kwa wadau wapenda maendeleo na italifanyia kazi kiufasaha na kwa wakati.
Akiongea mara baada ya hotiba ya mgeni rasmi Rais wa Chama cha Walimu (CWT) Taifa Leah Ulaya amesema suala la ubadhilifu katika mitihani limepungua kwa kiwango kikubwa na hiyo ni ishara kuwa walimu wanawajibika na kuheshimu misingi ya taaluma yao.
Amesema mbali na mafanikio hayo bado zipo changamoto mbalimbali ambazo ana imani zitatatuliwa huku akisisitiza suala la upandishwaji wa madaraja na nyongeza ya mishahara kwa walimu kufanyiwa kazi kwa wakati.
“Jambo hili mchakato wake huwa unaenda taratibu na sioni sababu kama mwalimu kapandishwa daraja halafu wahusika wa upandishaji madaraja wapo aratibu inabidi wawajibike kwa wakati ili kuongeza ufanisi kwa mwalimu,” amesisitiza Bi. Ulaya.
Mkutano huo umehusisha wadau kutoka kanda na mikoa mbalimbali, Wizara ya Elimu, Baraza la Mitihani, Walimu wa shule za Sekondari na Msingi.