Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali, Jacob Kingu amewataka watendaji wa Idara ya Huduma za Uangalizi, Jeshi la Polisi na Magereza kushirikiana kwa pamoja ili kupunguza msongamano wa wafungwa Magerezani.

Ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Maafisa Wafawidhi wa Mikoa waliokutana mkoani Morogoro, kwa lengo la kutathmini utendaji kazi wao zikiwemo mafanikio pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema kuwa, Idara ya Huduma za Uangalizi zamani ilikuwa ikiitwa Huduma kwa jamii ambayo ndio inayohusika na utoaji wa adhabu mbadala wa vifungo Magerezani, imeanzishwa ili kuhakikisha kuwa wafungwa wenye makosa madogo yasiyo hatarishi kwa jamii na taifa, wanatumikia adhabu zao kwenye jamii nje ya magereza.

“Kwa kufanya hivyo kungesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano Magerezani hivyo kuipunguzia Serikali  gharama za kuwahifadhi wafungwa Magerezani,” amesema Meja Jenerali Jacob Kingu.

Aidha, amewataka watendaji hao wa Idara ya Huduma za Uangalizi kubainisha changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ili ziweze kutatuliwa kwa haraka, jambo litakalosaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi hivyo kupunguza msongamano wa wafungwa Magerezani.

Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo amemuagiza Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Uangalizi, Aloyce Musika kupeleka watendaji katika mikoa mitatu, Lindi, Katavi na Ruvuma ili wakazi wa mikoa hiyo waweze pia kupata huduma zinazotolewa na Idara hiyo, kwani kwa sasa Idara hiyo ina watendaji wawakilishi katika Mikoa 23 hapa Tanzania.

Meek Mill amapa ushauri Tekashi 69, 'asijifanye mgumu'
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Novemba 30, 2018

Comments

comments